Washitakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo, Jumatatu ya wiki hii na kusomewa mashitaka hayo huku muda mwingi wakionesha kujutia kosa hilo ambalo hawakujua kama ni bomu ambalo litakuja kulipuka.
Muda mwingi, Mvungi akiwa mahakamani hapo alikuwa akiweka mikono juu ya kichwa (angalia picha) jambo lililotafsiriwa kwamba ni kuonesha kujutia tukio hilo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alisema washitakiwa walitenda kosa hilo kati ya Desemba, mwaka 2010 na Mei, mwaka huu katika Mtaa wa Azimio Kata ya Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Wakili huyo alidai kuwa katika kipindi hicho, washitakiwa wakiwa walezi wa mtoto Nasra, walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na hivyo kumsababishia magonjwa mbalimbali.
Maradhi yaliyotajwa kumkumba mtoto huyo akiwa ndani ya boksi ni utapiamlo, maumivu ya kifua na mvunjiko wa mifupa katika mwili.
Hata hivyo, licha ya dhamana kuwa wazi, hakuna mtu aliyejitokeza kuwadhamini washitakiwa hao hivyo kurejeshwa gerezani huku watu wakishangilia kwa kusema kwamba kitendo walichokifanya hawastahili kurejea uraiani.
0 comments:
Post a Comment