Tuesday, 3 September 2019

Serikali Yaridhia Ombi La Kuwapatia Ardhi Vijana Waliohitimu Mafunzo Nchini Israel

...
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Jerusalem,Israel
Serikali imeridhia ombi la vijana 45 waliohitimu masomo ya Kilimo nchini Israel la kuwapatia ardhi kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta ya Kilimo.


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo  tarehe 2 Septemba 2019 wakati akizungumza na vijana hao wakati wamahafali ya mafunzo ya Kilimo ya Agro Studies yaliyofanyika jijini Jerusalem nchini Israel na kuwatunuku vyeti vya kuhitimu wanafunzi 45 kutoka Tanzania.

Amesema kuwa serikali ya Tanzania ina ardhi nzuri yenye rutuba ambayo haijaguswa kwa ajili ya kilimo hivyo huo ni muda mwafaka kwa vijana hao kupatiwa ardhi kwa ajili ya kuonyesha kwa vitendo waliyofundishwa wakati wa masomo yao nchini Israel.

Alisema kuwa ni wakati muafaka kwa wanafunzi hao kutumia ujuzi walioupata wa kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ili kutoa elimu ya kilimo hicho nchini mwao pindi watakaporejea.

Amesema kuwa nafasi hizo za masomo ya kilimo nchini Israel zimetoa fursa kwa wataalam hao kuongeza ufanisi katika Sekta ya kilimo hivyo watakaporejea nchini wanapaswa kukibadilisha kilimo kuwa na tija zaidi.

Aidha, amesema kuwa, tatizo kubwa la Sekta ya Kilimo nchini ni uzalishaji mdogo usiokuwa na tija ambapo wakulima hutumia nguvu kubwa lakini matokeo yanakuwa madogo. hivyo, amesisitiza kuwa, watakaporejea nchini Tanzania wanatakiwa kutoa elimju kwa wakulima ya kuzingatia mbinu bora za kilimo, matumizi sahihi ya pembejeo, mbolea na pia kutumia mbegu bora ili kuweza kumnufaisha mkulima.

Aliongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kwa kiasi kikubwa Sekta ya Kilimo hivyo ni muhimu kilimo cha umwagiliaji kikaanza kutumika maeneo mbalimbali ya nchi kwa sababu ya uwepo wa vyanzo vya maji vya kutosha na sio kuendelea kutegemea kilimo cha mvua ili kupambana na hali hiyo.

“Hadi sasa eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji ni hekta 475,000 na Mkakati wa Serikali ni kufikia hekta milioni moja ifikapo mwaka 2035,”amesema Mhe Hasunga.

Hata hivyo, Waziri Hasunga amesema kuwa ataiomba Serikali ya Israel kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza bonde la mto rufiji kwa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili wakulima wengi waachane na kilimo cha kutegemea mvua kama ilivyo sasa.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger