Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano jana walishindwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza shauri linalowakabili ikielezwa kuwa basi la Magereza limeharibika.
Maimu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 100, likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 7/2019.
Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally alieleza kuwa, wamepewa taarifa na askari magereza kuwa basi linalowabeba washtakiwa hao kutoka gereza la Segerea kuelekea mahakamani hapo ni bovu.
Kutokana na hali hiyo Swai aliiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.
Hakimu Ally baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 14 itakapotajwa tena.
Mbali na Maimu Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi, mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, ofisa usafirishaji, George Ntalima, mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Kati ya mashtaka yanayowakabili, 24 ni ya kutakatisha fedha, 23 ya kughushi, 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na matano ya kuisababishia hasara mamlaka hiyo.
Mengine ni mawili ya kula njama ya kulaghai, mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.
0 comments:
Post a Comment