Tuesday, 23 April 2019

Profesa Lipumba Amkumbuka Kikwete....Aitaka Serikali Iruhusu IMF Ichapishe Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Tanzania

...
Mwenyekiti wa Chama cha Civic Union Front (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba,  amesema kitendo cha serikali kukataa taarifa ya Shirika la Fedha  Duniani (IMF) isichapishwe ni sawa na serikali kujipiga risasi yenyewe kwani maswali ni mengi yanayohusu kwa nini serikali inazuia taarifa hizo kuchapishwa.
 
Prof. Lipumba amesema hayo katika mkutano wake na wanahabari leo Aprili 23, ambapo amebainisha kuwa kuzuiwa kwa ripoti hiyo kutazorotesha mahusiano ya taifa na shirika hilo na kudai kuwa wakati wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete hakukuwepo na zuio lolote.

“Ni vyema taarifa ya Shirika la Fedha la Dunia (IMF) ikachapishwa ili wabunge wakaisoma na kama kuna mapungufu wakasema ni wapi kuna mapungufu ili irekebishwe. Riba za mikopo katika mabenki bado ziko juu sana, hii inapunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.

“Namshauri Waziri wa Fedha, Dkt. Mpango aruhusu taarifa hiyo ichapishwe ili Watanzania na wabunge waisome na kama kuna matatizo serikali inaweza ikatoa msimamo wake. 


"Huenda katika taarifa yao, IMF wanatoa sababu za kwa nini uchumi wa Tanzania utaporomoka, ni vyema serikali ikaruhusu huu uchambuzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa ili tujue watu wengine wanatazamaje uchumi wetu na kama kuna ubovu basi turekebishe.

“Rais Jakaya Kikwete aliendeleza mahusiano mazuri na IMF, japo watu walikuwa wanamsema kuwa ni mzee wa kutembea nchi za nje lakini IMF waliweza kuja kufanya mkutano mkubwa hapa kwetu mwaka 2009. 


"Wakati huu tunaojadili bajeti bungeni ni vizuri ripoti ya uchambuzi wa IMF ichapishwe ili wabunge wapate kuisoma na kujua kama sera zetu zinakidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi wetu au la!

“Katika utawala huu kumekuwa hakuna programu yoyote ya Shirika la Kimataifa, programu ya mwisho ilikuwa mwaka 2014 wakati Rais alikuwa Jakaya Kikwete. Unapokuwa hauna programu kubwa za kimataifa kama hii ya IMF, wale wanaotaka kukukopesha wanakuwa na mashaka kidogo, na wakitaka kukukopesha wanakupa mikopo yenye riba kubwa.

“Siyo kwamba unalazimishwa kutekeleza jambo fulani, ni suala la uchambuzi wa hali ya kiuchumi, sasa kusema ni suala la ubeberu siyo sahihi kwani mpaka sasa sarafu ya China imeingizwa kwenye kikapu cha IMF,” amesema Lipumba.

 
Aidha wakati hayo yakijiri, Waziri wa Fedha, Dkt. Phillip Mpango amelieleza Bunge leo  April 23, 2019 mjini Dodoma kuwa Serikali iko katika majadiliano na IMF kuhusu ripoti ya Tanzania na kuna siku 14 za kujadiliana kufuatia wataalamu waliotumwa awali kutozingatia hoja za upande wa Serikali kama ulivyo utaratibu.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger