Monday, 29 April 2019

Mfumo Wa Taifa Wa Takwimu Za Mtakuwwa Kusaidia Kupunguza Ukatili Dhidi Ya Wanawake Na Watoto

...
NA: MWANDISHI WETU
Mfumo wa Taifa wa takwimu za MTAKUWWA utasaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Asanterabi Sang’enoi wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau mbalimbali kutoka  kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Mashirika ya Kimataifa na Asasi za Kiraia kujadili mfumo na nyenzo kwa ajili ya udhibiti wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto utakaohusisha ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa, kutoa taarifa na ufuatiliaji kilichofanyika katika ukumbi wa Umwema uliopo Mkoani Morogoro.

Alieleza kuwa lengo la mpango kazi huo ni kuboresha mifumo itakayo saidia kuwa na taarifa na uwepo wa takwimu sahihi ambazo zitasaidia kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo 2022.

“Uwepo wa mfumo huo utawezesha wadau kupata uelewa juu ya ukusanyaji wa taarifa na takwimu kwa kuandaa taarifa ambazo zitasaidia kupima maendeleo ya Mpango Kazi wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto hapa nchini,” alisema Sang’enoi.

Aidha aliwataka wadau wa kikao kazi hiko kushirikiana kwa pamoja ili waweze kuwa na mifumo ya taarifa sahihi na takwimu rasmi za ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Mathias Haule alieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto barani Afrika kwa na inaongoza kwa kuwa na mifumo mingi ya ulinzi kwa wanawake na watoto ikiwemo uanzishwaji wa madawati ya jinsia na watoto.

Naye, Bi. Lucy Tesha kutoka UN Women alisema kuwa alisema kuwa kikao kazi hiko kitamwezesha kila mdau kutambaua majukumu yake na kuweza kukusanya taarifa kwa kutumia mfumo mmoja ambao utakuwa na data sawia ambazo zitakuwa hazijirudi kama ilivyokuwa awali.

Pia, Mchumi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ni Mratibu wa Madawati ya Jinsia na Watoto Bi. Happiness Mugyabusi alifafanua kuwa mpango kazi utasaidia kuwa na takwimu za awali ambazo zitawezesha kutambua ndani ya miaka mitano ijayo Taifa lilivyopiga hatua katika kutatua masuala haya ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Nchi yetu ina programu nyingi zinazozingatia udhibiti wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini wadau wameshindwa kuratibiwa vizuri kwa kukosa mfumo sahihi wa kukusanya taarifa na hivyo kupelekea kuwaleta wadau kwa pamoja ili kuwa na taarifa na takwimu za pamoja na uratibu mzuri wa wadau wote wa masuala ya wanawake na watoto,” alisema Mugyabusi.

Katika kikao kazi hiko wadau mbalimbali waliweza kushiriki ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu ambao ndio waratibu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, MUHAS, Mashirika ya Kimataifa (UN – Women), Asasi za Kiraia ( Child Watch, WFT, TCRF, WILDAF, TGNP na TECDEN).


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger