YANGA SC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.
Shujaa wa Yanga SC leo ni mchezaji wake kipenzi cha mashabiki, Mrisho Khalfan Ngassa aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 13 akimalizia krosi nzuri ya kiungo mwenzake mshambuliaji, Ibrahim Ajibu Migomba.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 77 baada ya kucheza mechi 33 ikiendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 69 za mechi 27, wakati Azam FC inabaki nafasi ya tatu na pointi zake 66 za mechi 33.
Yanga SC leo iliingia na maarifa ya kucheza kwa makini zaidi, ikijilinda zaidi na kushambulia kwa kushitukiza, huku Azam FC wakionekana bora tangu mwanzo wa mchezo.
Na baada ya kupata bao lake hilo moja pekee la ushindi, Yanga SC ikazidisha mchezo wa kujihami na pamoja na Azam FC kuuteka mchezo na kushambulia zaidi, lakini hawakufanikiwa kupata bao.
Yanga ilipata pigo dakika ya 38 baada ya beki wake kushoto, Gardiel Michael kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, huku nafasi yake ikichukuliwa na Jaffar Mohammed.
Kipindi cha pili, kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliimarisha safu ya ulinzi kwa kumtoa Ajibu na kumuingiza kiungo wa ulinzi, Said Juma ‘Makapu’.
Washambuliaji wa Azam FC, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Daniel Lyanga pamoja na kiungo Mudathir Yahya wote walikosa mabao ya wazi leo.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Ennock Atta-Agyei dk76, Mudathir Yahya, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael/Jaffar Mohammed dk38, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Banka’, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu/Said Juma ‘Makapu’ dk76 na Raphael Daudi.
0 comments:
Post a Comment