Sunday, 28 April 2019

Chama cha wenye ulemavu wa Ngozi Tanzania (TAS) chalaani vitendo vya ufukuaji makaburi.

...
Chama Cha Watu Wenye Ualbino Tanzania kwa masikitiko kinauarifu umma kuhusu tukio la kaburi la marehemu Aman Anywelwisye Kalyembe mwenye Ualbino, aliyezikwa mwaka 2015 kufukuliwa usiku wa kuamkia tarehe 23/4/2019 katika kijiji cha Ibililo kata ya Nkunga wilayani Rungwe ambapo wahusika waliondoka na masalia ya viungo vya marehemu. 

Tukio hili la tatu kwa mkoa wa Mbeya limeibua simanzi na hofu kwa  Watu Wenye Ualbino na familia zao, kwa uzoefu kuwa linahusishwa na imani za kishirikina hasa kipindi hiki tunapoelekea mwaka wa uchaguzi 2020. Ni ishara wazi ya ukatili kwa Watu Wenye Ualbino si tuu wakiwa hai bali hata wakiwa wafu.

Chama cha watu wenye ualbino Tanzania kinaungana na wadau na wote wenye mapenzi mema kukemea vikali tukio hili ovu. 

Ni tukio ambalo limejitokeza wakati baadhi ya wenzetu wako katika vituo maalum, huku kiu yao na jitihada za serikali na wadau wengine ikiwa ni kuona wanarejea kuishi na familia zao, ndugu zao, marafiki na jamii zao katika maeneo yao. 

Tukio hili  linarejesha hofu kwa Watu Wenye Ualbino na familia zao kwani ni tukio la 23 la vitendo ovu vya ukiukwaji wa heshima ya makaburi ya watu wenye ualbino likihusishwa na imani za kishirikina.

Watu Wenye Ualbino na familia zao watafurahi kuona serikali inachukua hatua stahiki kwa wakati ili matokeo mazuri tuliyokuwa tumeyafikia, yakiwemo: watoto wenye ualbino kuanza kuandikishwa shule za kawaida ndani ya maeneo yao na vituo vingi vikiwepo Buhangija (Shinyanga) na Kabanga (Kigoma) kuanza kupunguza idadi ya watoto na watu wazima wenye ualbino, yawe endelevu.

Tunamwomba Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia kati suala hili, ikiwa ni kutumia nafasi yake kukemea uovu huu na kuwezesha kifedha mikakati iliyopo na itakayokuwepo yenye nia ya kukomesha uovu huu dhidi ya Watu Wenye Ualbino na zaidi  jamii ipate hamasa na kuziacha fikra potofu na matendo ya kishirikina.

 Miongoni mwa mipango tunayoomba iwezeshwe na serikali ni pamoja na:
1.    Mpango kazi wa kutokomeza mauaji na ukatili wa watu wenye ualbino Tanzania uliondaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na wadau wengine.
2.    ‘Cross-Border Cooperation Plan on Preventing and Combating Trafficking and the Protection of Persons with Albinism in Malawi, Tanzania and Mozambique’ Ulioandaliwa na International Organisation for Migration (IOM), serikali kwa uwakilishi kupitia wizara ya Mambo ya Ndani  na wadau wengine.
3.    ‘Joint Programme for the Protection and Wellbeing of People with Albinism in Tanzania’ Ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu wa UNESCO kwa ushirikiano na wadau wengine.
4.    ‘ACTION STRATEGY: Minorities and Other Vulnerable Groups’ ulioandaliwa na Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) kwa ushirikiano na wadau wengine.   
5.    ‘Regional Plan of Action on Albinism adopted on May 22, 2017 by the African Commission on Human and Peoples' Rights’ ulioandaliwa na mtaalamu wa kujitegemea wa UN akisimamia haki za watu wenye ualbino.

Tunaitaka serikali katika ngazi zote wakati huu wa kuelekea chaguzi za serikali za vijiji na mitaa na kwenye uchaguzi mkuu mwakani 2020 kuweka ajenda ya hamasa kwa jamii kuhusu ualbino na athari za vitendo vya kishirikina kwenye kampeni zao. 

Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri na ya kupongezwa kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita. Juhudi zao zimechangia kupungua kwa matukio. Mafanikio haya yamechangiwa pia na jamii kutoa ushirikiano hivyo tunaomba mtu yeyote mwenye taaifa yoyote kuhusiana na matukio haya afikishe jeshi la polisi au awasiliane nasi kwa wakati ili kufanikisha kuwakamata watu hawa waovu. Tunamsihi sana IGP Simon Sirro kuongeza kasi hasa katika upelelezi na kushiriki katika mchakato wa kuelimisha na kuhamasisha jamii kulinda na kuheshimu utu na uhuru wa Watu Wenye Ualbino na familia zao.

Mahakama zina mchango mkubwa kukomesha mauji kupitia adhabu kali ili iwe kama elimu na fundisho kwa jamii. Watu Wenye Ualbino wana imani na Mheshimiwa Jaji Mkuu na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla wakitarajia kwamba kesi zilizochukua muda mrefu zitashughulikiwa ziishe kwa wakati sanjari na adhabu stahiki kutolewa kwa watakaobainika kuwa na hatia.

Kutokana na matukio haya, Watu Wenye Ualbino na familia zao ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari stahiki kwa ajili ya ulinzi wao wakati wote. Toa taarifa polisi na au mamlaka za karibu mapema iwezekanavyo uonapo kiashiria chochote cha uhalifu ili jitihada za kuzuia zifanikiwe.

Vyombo vya habari, viongozi wa dini, serikali kupitia viongozi wa kisiasa, Wizara na taaisi nyingine za kiserikali na za kiraia tuongeze juhudi hasa katika elimu kwa jamii kwa njia mbalimbali ambazo ni endelevu, hii itasaidia sana kuibadili jamii kifikra  ili hatimaye utu wa mtu mwenye ualbino uthaminike.

Mungu ibariki Tanzania

Nemes Colman Temba
Mwenyekiti – Taifa
Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania
Aprili 27, 2019

Kwa mawasiliano
Simu (ofisi): 022 2110527
Mob. (Mwenyekiti): 0784 874 592
Email:   info@tas.or.tz




Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger