Sunday, 28 April 2019

Waziri Mkuu Aagiza Mabango Ya Utalii Yawekwe Uwanja Wa Ndege Wa KIA

...
*Ni yenye kuonyesha wanyama, milima, fukwe, mambo ya utamaduni

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa bodi ya KADCO uhakikishe unaweka mabango ya kielektroniki yenye kuonesha vivutio vya utalii kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“KADCO na Wizara ya Maliasili na Utalii, shirikianeni kuweka utaratibu wa kutangaza vivutio vyetu vya utalii hasa wanyama kwenye viwanja vyote vya ndege. Tunazo mbuga, milima, fukwe za bahari na ngoma za makabila mbalimbali, wekeni mabango yanayobadilisha picha.”

“Screens zenye wanyama wanaobadilikabadilika zinaleta mvuto lakini pia ni fursa ya kutangaza vivutio vyetu. Nimezunguka humu ndani, kuta zote ni nyeupe tu, tumieni fursa hiyo kutangaza tamaduni zetu na vivutio tulivyonavyo," Waziri Mkuu alimweleza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO), Mhandisi Christopher Mukoma.

Alitoa agizo hilo jana mchana (Jumamosi, Aprili 27, 2019) wakati akikagua miundombinu ya uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) mara baada ya kuwaaga watalii 274 kutoka Israeli wanaowawakilisha wenzao 1,000 walioondoka nchini jana kurejea kwao.

Akiwa uwanjani hapo, Waziri Mkuu alikagua eneo la mapokezi, sehemu ya abiria wanaoondoka na wanaowasili, sehemu ya uhamiaji, mashine za kukagua mizigo ya wanaoondoka na wanaowasili, sehemu za kutolea huduma na maduka.

Pia alimwagiza Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji kwenye kiwanja hicho cha ndege, Bw. Filbert Ndege awasiliane na makao makuu yake ili waangalie uwezekano wa kuongeza madirisha ya kutolea huduma za uhamiaji (counters) ili huduma hiyo itolewe kwa kasi zaidi.

“Angalieni cha kufanya, ikibidi eneo hili lipanuliwe na counters nyingine ziongezwe ili kufast-track utoaji wa huduma hasa msimu ambao watalii wengi huingia nchini.”

Pia aliwataka KADCO waboreshe eneo la maegesho ya magari kwa kufanya upanuzi na kujenga maturubai ya vivuli (shades) ili kuyakinga na jua kali magari ya wateja.

(mwisho).

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, APRILI 28, 2019.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger