Monday 1 February 2016

Nelly Muosha Magari wa Posta-24

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale fundi Yassin alipomfahamisha Doreen kwamba kwa siku ile walimaliza kazi ndipo mtoto huyo wa kishua aliwapa pole akaingia ndani alikochukua bahasha ya khaki na kumkabidhi fundi huyo. Je, kilifuatia nini? Songa mbele na chombezo hili lisiloisha utamu…
Kwa vile alijua ulikuwa ‘mpunga’ wa maana, fundi Yassin alitabasamu na kumshukuru Doreen aliyemwambia asijali, kama ilivyokuwa kwa fundi, Zakayo, Haruni na Nelly nao walitabasamu kwani walijua mifuko yao ingetuna.
Baada ya kuagana na Doreen, fundi na vijana wake waliondoka lakini kabla ya kufika kituo cha daladala alifungua ile bahasha na kukuta ilikuwa na shilingi lakini 250,000.
Alimpatia Haruni shilingi 40,000, Zakayo 40,000 na Nelly shilingi 30,000 kisha vijana hao wakiwa na furaha walielekea kituo cha basi walikopanda gari, wa kwanza kuteremka alikuwa Haruni na walipofika Tegeta Kibaoni Zakayo kabla ya kumuaga fundi Yassin alisema:
“Kaka mkubwa kama nilivyokwambia, usipoufanyia kazi ushauri wangu kesho nikija itakuwa mara yangu ya mwisho kufanya kazi.”
Maneno ya Zakayo yalimwingia barabara fundi Yassin ambaye hakuwa tayari kumpoteza dogo huyo mchapakazi aliyekuwa akiijua kazi yake na wakati mwingine alipokuwa na dharura alikuwa akifanya kazi zake bila tatizo.
“Sawa kaka mkubwa nimekuelewa,” fundi Yassin alimwambia Zakayo bila Nelly kujua kama jambo hilo lilimhusu yeye.
“Kaka mkubwa, kwani Zakayo kakupa ushauri gani ambao anasema usipoufanyia kazi kesho ndiyo itakuwa mara yake ya mwisho kufanya kazi?” Nelly alimwuliza fundi Yassin.
“Ni mambo tu ya kawaida, nitakuambia,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Walipofika Kituo cha Kwa Ndevu, Nelly na fundi Yassin walipanda daladala la kwenda Ubungo ili pale waunganishe la Tandika, kwa kuwa walipandia mwanzo walikaa katika siti moja.
Safari yao ilikuwa nzuri sana kwani haikuwa na foleni hadi Ubungo walikopanda gari la Tandika, njiani walikuwa wakizungumza mambo mchanganyiko yakiwemo ya mademu lakini fundi Yassin hakupenda kumuweka wazi kuhusu jambo alilokuwanalo moyoni.
Walipoteremka Tandika, fundi Yassin alimpeleka sharobaro Nelly kwenye baa moja ambapo alimwambia aagize kinywaji chochote alichohitaji pamoja na chakula.
Nelly aliagiza kilevi alichokuwa akitumia pamoja na chipsi na mishkaki mitatu, fundi Yassin aliangiza soda na kongoro pamoja ndizi mbili wakaanza kujiburudisha.
“Dogo, samahani kuna jambo nataka kuzungumza na wewe lakini lichukulie kawaida kwani ndiyo changamoto za maisha,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Nelly alipoambiwa hivyo, alishtuka na kumwuliza fundi Yassin ni jambo gani hilo ndipo akamwambia anashukuru kwa kuwa pamoja naye kule site kwa siku mbili lakini siku ile ilikuwa ya mwisho kuendelea kufanya kazi kule.
Nelly alipoambiwa hivyo alimwuliza kwa sababu gani ndipo fundi huyo akamwambia kila kitu kuhusu uwezo wake kikazi na jinsi alivyomzoea haraka Doreen na nyumba ya bosi wake jambo ambalo lilikuwa hatari kwake.
“Kama ulivyomsikia Zakayo akisema kama sitaufanyia kazi ushauri wake ataacha kazi, jambo lenyewe ndiyo hili ninalokueleza ndiyo maana nimeona nikwambie ukweli mdogo wangu,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
“Yaani aliyependekeza unifukuze kazi ni Zakayo si ndiyo?” Nelly alimwuliza fundi wake.
“Siyo kapendekeza, tumeona hatari iliyopo mbele yetu kwa bosi, wewe kuwa mpole kama hela za matumizi nitakuwa nakupa wakati ukiangalia nini cha kufanya,” fundi Yassin alimwambia Nelly.
Pamoja na kauli ya fundi Yassin, Nelly alimmaindi sana Zakayo kwani alijua yeye ndiye aliyemchongea na kujisemea moyoni kwamba ‘watu wengine bwana wana roho mbaya, yaani mimi kuzoeana na mtoto wa bosi kuna ubaya gani?’
“Oke bro kwa kuwa umeamua hivyo poa tu!” Nelly alimwambia fundi Yassin.
“Siyo nimeamua, wewe kuwa mpole kama nilivyokwambia wala usimmaindi mtu yeyote,” fundi Yassin alimwambia.
Kufuatia alichoelezwa na fundi wake, Nelly alikosa raha hata bia aliyokuwa akinywa aliiona chungu, akawa anamfikiria Doreen huku akijisemea moyoni kwamba ndiyo atamkosa.
Kwa vile jambo hilo lilimchanganya akasahau kabisa kama alikuwa amepewa simu na binti huyo wa kishua hadi aliposhtuliwa na fundi Yassin aliyemwita.
“Dogo naona uko mbali kabisa,” fundi Yassin alimwuliza.
“Bro we acha tu, unajua tayari nilishaanza kuizoea kazi na kuifurahia sasa umenikatili sana wewe hujui tu!” Nelly alimwambia fundi Yassin huku moyoni akiwa na lake jambo.
“Usiwaze sana mdogo wangu, nitakapoanza kazi site nyingine tutaenda wote,” fundi Yassin alimwambia.
Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo. Maoni, ushauri nicheki kwa namba hiyo juu.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger