Monday 1 February 2016

Jini Mauti-20

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nilisema huku nikilia mno. Hawakuniambia kitu chochote kile zaidi ya kuondoka. Katika kipindi chote hicho sikuwa nikijua kwamba bibi yangu aliniwekea jini mauti mwilini mwangu na kwamba kwa kila mwanaume ambaye ningefanya naye mapenzi ilikuwa ni lazima afariki dunia. Endelea….
Siku iliyofuata, nilikwenda shuleni kama kawaida, nilipofika, nikaanza kusikia vilio kutoka kwa wanafunzi mbalimbali, moyoni niliumia mno, nilijua fika kwamba kile kilichokuwa kikiwaliza ni kuhusu kifo cha Mudi aliyefariki dunia mbele ya macho yangu.
Nikashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kunibubujika, nilihisi moyo wangu kuwa na maumivu makali mno. Sikuamini kama nilikabidhiwa umalkia ambao ulinifanya kumuua mwanaume yeyote ambaye ningelala naye.
Moyo wangu ukakosa amani kabisa, nilipokuwa nikiwaangalia walimu na wanafunzi waliokuwa wakilia, moyo wangu ulijisikia hukumu sana. Wengi walijua kwamba nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mudi lakini hakukuwa na aliyefahamu kama jana usiku tulikuwa wote hivyo kuona kwamba nisingeweza kugundulika.
Kitu kilichonishangaza ni wanafunzi wengi kuanza kuninyooshea vidole. Kwanza nikashangaa, haikuwa kawaida hata kidogo, kwa nini sasa waninyooshee vidole? Niliwafanya nini mpaka kunifanyia kitu kama hicho, kila nilichojiuliza, nikakosa majibu kabisa.
Sikutaka kujali sana, nikazidi kuendelea mbele mpaka nilipoingia darasani, huko nako kila mwanafunzi aliogopa kunisogelea ni marafiki zangu wawili tu ndiyo walionifuata, alikuwa Anita na Maria.
“Mbona watu wananikimbia na kuninyooshea vidole?” niliwauliza huku nikilia.
“Wanasema wewe ndiye umemuua Mudi,” alinijibu Anita.
“Mimi nimuue Mudi?”
“Ndiyo! Wanasema haukuanza kuua hapo, hata ulipokuwa na Thomas, ilikuwa hivyohivyo, alikufa kifo kama hiki, tena chumbani kwake,” alisema Maria, maneno yale yakaniongezea uchungu.
“Yaani mimi nimuue Mudi?” niliuliza kwa sauti ya juu na kuanza kulia.
Ndiyo nilimuua lakini sikujua nilimuua vipi. Wanafunzi waliniogopa sana na wengi wakayaamini maneno aliyokuwa akiyapakaza Agape kwamba nilikuwa mchawi. Kuanzia siku hiyo sikuwa na amani na hata nilipotaka kwenda mazishini na wanafunzi wengine, wote wakanitenga.
Niliachwa shuleni nikilia peke yangu, kilio changu kilikuwa ni kumlilia bibi yangu kwa kile alichokuwa amenifanyia. Sikutaka kabisa kuua, watu wote waliokuwa wamefariki dunia walikuwa wale niliowapenda kwa moyo wa dhati.
Hakukuwa na wa kunibembeleza tena, kila mtu alinikimbia na hawakutaka hata kunisogelea. Nilijisikia aibu kubwa, shule ikawa chungu, kuanzia siku hiyo nikajuta kuwa mchawi, sikuwa na uhuru hata kidogo, sikuwa na uhuru wa kuwa na mwanaume yeyote.
Wakati nikikaa hapo darasani huku nikilia tena shule nzima kukiwa hakuna mtu yeyote zaidi ya mlinzi, ghafla nikaanza kusikia kizunguzungu kikali, nikajikaza lakini ikashindikana kabisa, kizunguzungu kile kikanipelekesha mno, nikajaribu kusimama, nikashindwa, nikaangukia viti na hapohapo nikaanza kuona giza, sikujua tena ni kitu gani kiliendelea.
***
Nilikuja kupata fahamu na kujikuta nikiwa kitandani, dripu ilikuwa ikining’inia juu yangu na maji yalikuwa yakiingia taratibu katika mshipa wangu. Macho yangu yalikuwa mazito, kitendo cha kuiona dripu ile tu nikajua kwamba mahali nilipokuwa palikuwa ni hospitalini.
Nikaanza kuangalia huku na kule mle chumbani nilimokuwa peke yangu. Nikaanza kuvuta kumbukumbu ilikuwaje mpaka nikafika hapo pale.
Itaendelea wiki ijayo.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger