Monday 11 August 2014

MCHUNGAJI MTIKILA AANZA UKOFOFI !!! AKUKUSANYA SAINI ZA WATANZANIA ILI KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI KUPINGA BUNGE MAALUM LA KATIBA MPYA KUENDELEA MJINI DODOMA.

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY

 Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.       


Dar/Arusha. Joto la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), linazidi kupanda nchini baada ya wabunge na vyama vya siasa kuendelea kusisitiza kuwa Bunge hilo halina tija kwa taifa.

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amesema ameanza kukusanya saini za Watanzania wanaopinga kuendelea kwa Bunge hilo ili kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania, kusitisha vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.
Mchungaji Mtikila akizungumza na Mwananchi Jumapili alisema mchakato wa kukusanya saini hizo unaendelea katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Geita, Kagera, Dar es Salaam huku akibainisha kwamba mwitio wa watu ni mzuri.
“Natafuta saini 20,000 za Watanzania na sasa tayari tumekusanya saini zaidi ya 10,000 katika mikoa kadhaa na natarajia Watanzania wataendelea kuniunga mkono ili kuhakikisha mchakato huu. 

Nakwenda kuuzuia Mahakama Kuu na ninajua tu nitashinda,” alisema Mchungaji Mtikila.
Alisema anakusanya saini hizo ili kudhihirisha kuwa Watanganyika hawataki muungano, kwani mwaka jana Wazanzibari walikusanya maoni 1,946 ya kupinga muungano.
Dk Chegeni
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dk Raphael Chegeni alisema kuendelea kwa Bunge hilo bila kuwepo kwa Ukawa ni kuchezea fedha za umma.
Dk Chegeni alisema hayo jijini Arusha alipokuwa akihudhuria vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwamba kuendelea na Bunge hilo ni kucheza kamari ya hatari ambayo baadaye inaweza kusababisha malalamiko kwa wananchi na kuwagawa wananchi.
“Sioni sababu ya haraka, huwezi kuandika katiba bila ya maridhiano, haya mambo yenye utata itabidi yapatiwe muda mwafaka na mchakato huu kuendelea baada ya uchaguzi mkuu mwakani.”
Dk Chegeni alisema, kwa kuwa kuna mahitaji ya haraka yanayopaswa kuingizwa katika Katiba, ni busara Bunge la Novemba kutumika kufanya mabadiliko hayo, ambayo ni pamoja na kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, kuruhusu mgombea binafsi na pia kuingiza masuala ya haki za binadamu kwenye Katiba.
Alisema hadhani kama kuna haraka sana wa kuandika katiba wakati kuna kutoelewana, kwani Katiba inaweza kuandikwa hata na utawala ujao, ingawa nia nzuri ya Rais Jakaya Kikwete ilikuwa ni kuwaachia Watanzania Katiba Mpya.
Akizungumzia malumbano juu ya watu wanaotoa maoni ya mchakato wa Katiba nje ya Bunge hilo, alisema wanapaswa kuachwa kwani ni haki ya kila Mtanzania kutoa mchango wake ili kuwezesha kupatikana Katiba mpya.

“Hawa wazee wetu kina Jaji Joseph Warioba waache wazungumze na waendelee kutoa maoni kwani wanayo haki hiyo,” alisema Dk Chegeni mmoja wa makada vijana wa CCM.
Filikunjombe
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amenukuliwa na kituo kimoja cha Televisheni nchini akisema kuwa haungi mkono hatua iliyofikiwa na wajumbe wenzake wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu suala la Katiba halina mshindi na pia ni matumizi mabaya ya wingi wao ndani ya Bunge hilo.
Alipopigiwa simu na gazeti hili ili atoe ufafanuzi kuhusu kauli hiyo alisema: “Nitazungumzia hilo suala nikifika Dar es Salaam.”
Said Juma Nkumba
Kiongozi wa kundi la Tanzania Kwanza kutoka CCM, Said Juma Nkumba alisema kitendo cha baadhi ya wabunge wa CCM kuelezea misimamo yao ni ishara kwamba CCM haina msimamo katika hili.
“Hapo ndipo utaona kwamba CCM inazingatia demokrasia ya watu au mtu binafsi, haiwezi kumzuia mtu kutoa maoni yake kwani hiyo ndiyo demokrasia,” alisema Nkumba ambaye ni mbunge wa Sikonge (CCM).
Aliongeza: “Suala hili la Katiba lina uhuru wa mawazo kwa kila mtu kusema chochote na ndiyo msingi wa demokrasia.”
Shinikizo la kutaka kusitishwa kwa Bunge hilo lilianzishwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba Jumanne iliyopita wakati akichangia mjadala wa mabadiliko ya kanuni.
Alilitaka Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili.
Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya, hakiwezi kueleweka kwa Watanzania.
Pia, akizungumza na gazeti hili juzi, Nchemba alisema anaamini wapo wajumbe wengi kutoka CCM wanaomuunga mkono, ingawa hawajapata nafasi ya kuzungumza.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye Alhamisi iliyopita alijibu akisema kauli ya Nchemba ni mtazamo wake binafsi na hakuongea kama kiongozi wa chama hicho.
Wabunge wengine wa CCM waliotoa kauli za kumuunga mkono Nchemba ni pamoja na Alli Keissy (Nkasi Kaskazini), James Lembeli (Kahama) na Esther Bulaya (Viti Maalumu).
TLS
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura alisema chama hicho kinafuatilia kwa makini kujua athari za kuendelea kwa Bunge lenye wajumbe wa upande mmoja.
“Tunajiuliza je, endapo Katiba ikipatikana nini athari zake kisiasa. Hapo ndipo tunakwenda mahakamani kuitaka Mahakama itoe tafsiri ya vifungu vya sheria ili kujiridhisha uhalali wa Bunge hilo kuendelea,” alisema Rwechungura.
Aliongeza: “Mahakama ikishagundua upungufu tutaiomba mahakama iusimamishe kwani utakuwa si halali na hauna tija kuendelea.”
LHRC
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo- Bisimba alisema baadhi ya viongozi wanataka Katiba iliyopo ya mwaka 1977 iendelee kutumika.
“Wanauendeleza mchakato huu kwa lazima wakijua kuwa kuna watu watakwenda mahakamani ili wapate kisingizio kwamba tulitaka kuwatengenezea Katiba Mpya, lakini imezuiliwa,” alisema Dk Bisimba
Aliongeza, “ Kitendo hicho ndicho tunachokifuatilia kwa ukaribu, kwani Bunge hilo haliwezi kuendelea wakati kundi fulani halipo.”
ACT-Tanzania
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Tanzania, Samson Mwigamba alisema kuendelea kwa mchakato huo kama ulivyo inawezekana ikapatikana Katiba Mpya yenye uhalali kisheria, lakini ikakosa uhalali wa kisiasa au kijamii.

“Bunge Maalumu la Katiba lisimamishwe ili kuendelea kutoa fursa ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka na maridhiano,” alisema Mwigamba.
Aliongeza: “Mchakato wa kuandika Katiba Mpya uahirishwe hadi baada ya uchaguzi mkuu. Hivi sasa Bunge la Jamhuri linatakiwa kufanya marekebisho katika Katiba ya sasa ili kuuwezesha uchaguzi mkuu ujao 2015 uwe huru na wa haki.”
Baadhi ya maeneo ambayo Mwigamba aliyabainisha kufanyiwa marekebisho kuwa ni; Tume ya uchaguzi iwe huru na ionekane kuwa huru na kuruhusu mgombea binafsi na mbunge akitaka kuhama chama ahame na ubunge wake.
Maeneo mengine ni: Kushuka kwa umri wa mgombea urais, kuweka sharti kwamba ili mgombea atagazwe kuwa Rais lazima apate angalau asilimia 50 ya kura zilizo halali na wagombea urais lazima washiriki midahalo mitatu wakati wa kampeni.MWANANCHI
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger