Mahabusu wa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha, jana walizua tafrani katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini hapa, baada ya kuvua nguo na kugoma kushuka kwenye basi wakipinga kitendo cha watuhumiwa wawili wa dawa za kulevya kuachiwa kinyemela.
Watuhumiwa
wanaolalamikiwa ambao mashtaka yao yalibadilishwa mara mbili ili wapewe
dhamana ni Dharam Patel (26) na Nivan Patel (20) wanaodaiwa kukamatwa
na kete 173 za heroini na misokoto 300 ya bangi, Aprili mwaka huu.
Mahabusu
hao walikuwa wakipaza sauti kupinga madaraja kati ya wenye nacho na
wasio nacho kwa wengine kuachiwa na wengine kubaki ndani kwa kisingizo
cha ‘upelelezi haujakamilika’.
Huku
wakipaza sauti zao kwa nguvu, mahabusu hao wa kesi za mihadarati
ikiwamo mirungi na bangi, wizi wa kutumia silaha na mauaji, walisema
wamekaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili, lakini hawajawahi hata
kusomewa maelezo ya awali na kuendelea kuteseka gerezani.
Sauti ilisikika kutoka ndani ya basi: “Wenzetu hata mwezi haujaisha wanafutiwa kesi, jamani sisi tumekosa nini? Tunataka haki itendeke kwa wote.”
Mahabusu hao walionekana wakiwa wamesimama ndani ya basi hilo bila nguo, huku umati wa watu waliofika mahakamani hapo ukitazama.
Baada
ya kuona umati wa watu unazidi kuongezeka kuwashangaa mahabusu hao,
askari wa magereza waliondoa basi hilo eneo la Mahakama.
Kuachiwa watuhumiwa
Taarifa
za kuachiwa kwa watuhumiwa hao wa dawa za kulevya waliokuwa na kesi
mbele ya Hakimu Mkazi Arusha, Mwakuga Gwanta zilidaiwa kuwa zilitokana
na Ofisi ya DPP Arusha, kubadilisha hati ya mashtaka.
Ilidaiwa
kuwa badala ya kudaiwa kuwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya,
iliandikwa kuwa walikutwa na dawa hizo mashtaka ambayo yana dhamana.
Kamanda
wa Kikosi cha Polisi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema
jana kuwa ofisi yake haina taarifa za watuhumiwa hao kupewa dhamana
lakini alisema kulikuwa na jaribio hilo.
“Ninachojua
kesi hii ilipangwa kutajwa Aprili 29, mwaka huu, lakini ikasogezwa
mbele hadi Mei 2 na kilichofanyika hati ya mashtaka ilibadilishwa na
kuandikwa wamepatikana na dawa za kulevya."
Alisema
kwa mujibu wa sheria, mtu ambaye anakamatwa na dawa za kulevya zenye
thamani chini ya Sh10 milioni anaweza kupewa dhamana, lakini kiwango
kikiwa zaidi ya hapo, hapati dhamana.
“Baada
ya kubainika kuna njama za mashtaka kubadilishwa, tulipinga kwa kuwa
kosa lipo wazi kwamba walikuwa wakisafirisha dawa hizo, sidhani kama
wamepewa dhamana... sidhani kama inawezekana ila tunafuatilia kwa karibu
tukio hili,” alisema Nzowa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kazi ya polisi
ilikuwa ni kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani tu.
Msajili
wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Wilibard Mashauri alisema hahusiki
katika malalamiko hayo kwa kuwa si mpelelezi wa kesi.
“Lakini
hawa mahabusu wanalalamikia kuachiwa kwa wale watuhumiwa wenye kesi ya
dawa za kulevya, kesi ambayo haipo kwangu wala sijui wameachiwa kwa
kifungu gani na inategemea na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DP)
amewaachia kwa kifungu gani,” alisema.
0 comments:
Post a Comment