Friday 2 May 2014

CHID BENZ NA USTAA PORI

...
NI bwana mdogo, lakini ana mwili mkakamavu wenye kumuonyesha kama kijana mwenye ubavu. Ana sauti nzuri ya kukwaruza akiwa nyuma ya Mic, ambayo kwa mashabiki wa Hip Hop za Kimarekani, wanaweza kumlinganisha na rapa Ja Rule!
Namzungumzia Rashid Makwiro, maarufu kama Chid Benz, mtoto wa Ilala Maflet, aliyeingia katika anga la Bongo Fleva miaka michache iliyopita na kuteka mashabiki wengi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kurap.
Uwezo wake unadhihirishwa na jinsi alivyoweza kushirikishwa na wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya katika nyimbo zao. Unapowataja wasanii waliofanya kolabo nyingi, ni jambo gumu kumtupa nje ya Top Ten Chid Benz.
Anajua kuitumia sauti yake au kama wenyewe watu wa muziki wanavyosema, ‘ananata na beat’. Msikilize kwa mfano katika wimbo wa Mwasiti uitwao Hao au sikia kibao cha Tunda Man kiitwacho Neira. Kuonyesha anajua, amepiga hadi taarabu akiwa na Mzee Yussuf katika wimbo wa Mashalaah Raha za Dunia na Nampenda sana aliofanya na Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa.
Licha ya hizo za kushirikishwa, dogo pia amekamua mwenyewe katika nyimbo za kutosha kama Nakaza Roho, Kila Nnapokuona, Nipokee aliomshirikisha Ben Paul, Get Down (Nonini), Viini vya Macho (Solo Thang), Nimerudi (Dully), Dar Stand Up, Niaje na nyinginezo kibao.
Kifupi, Chid Benzi ni mmoja kati ya vijana wenye vipaji ambao taifa limewahi kuwapata. Katika nchi ambayo wasanii wangepata stahiki zao kiasi wanavyostahili, bila kuibiwa na wajanja wachache wanaolegezewa na serikali, huyu angekuwa mmoja wa mamilionea wakubwa kwa sasa.
Lakini nyuma ya sifa hizi, Chid ana tabia ya utukutu, tena ule wa kizamani, wa kupenda kupiganapigana ovyo na wenzake. Nilianza kumsikia mapema tu alipojiingiza katika Bongo Fleva akiwa bado hana jina kubwa, zilipotapakaa habari kwamba alimpiga Prof Jay.
Zilikuwa ni shutuma za kushtusha mno, ingawa siku moja nilipokutana nao wote wawili kwenye tukio moja la kisanaa pale JB Belmont jijini Dar, Chid alikataa kumpiga Jay na hata Jay alikataa kuwahi kupigana naye.
Najua walikwaruzana, lakini Prof alitumia utu uzima na busara kutolikuza jambo hilo.
Baada ya pale, mchizi ameendelea kuwa na matukio mengi yanayomhusisha na kupigana hadi mtu unapatwa na mshangao, kama kijana wa kisasa, aliyezaliwa, kukulia na kusomea Dar es Salaam, anaweza kuwa na mambo ya kizamani kama haya ya kupigana ngumi.
Juzikati aliripotiwa kupigana Maisha Club kama ilivyotokea siku kadhaa nyuma, alipodaiwa kutaka kupigana na msanii mwenzake Club Billicanas.
Lakini mbaya zaidi ni tukio lake la hivi karibuni, analodaiwa kumpiga na kumjeruhi vibaya msichana anayedaiwa kuwahi kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.
Kwanza, kijana wa kiume, mwenye umbo kakamavu kama la Chid, ni kujidhalilisha kumpiga msichana. Halafu, staa wa levo zake, ni vipi umdunde mwanamke hadharani kama wafanyavyo watemi wanaovuta bangi?
Nimshauri tu mdogo wangu Chid, naona kama umaarufu unamlevya. Katika dunia ya sasa, kupigana ngumi nje ya ulingo ni ushamba.
Watu hawapigani vibao usoni, wanapigana kujikomboa kimaisha, ili kesho maisha yawe rahisi kuliko jana.
Kuna wasanii wamekuwa maarufu tangu yeye anasoma, lakini hawajawahi kuripotiwa kuwa na upuuzi kama huu na bado hawafikii kimuziki wala kimaisha.
Enzi za ubabe wa kupandisha bega juu na kudunda kwa mikogo zilishapotea na haziwezi kurudi tena.
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger