-Hifadhi ya Taifa Ruaha yasema wanyama wanahangaika, samaki wameanza kufa
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV-Ruaha
IMEELEZWA kwamba Mto Mkuu Ruaha ambao ni kwa uhai wa hifadhi ya taifa ya Ruaha upo kwenye hali mbaya kutokana na maji yanayopita kwenye mto huo kukauka kabisa na hivyo kusababisha hata wanyama kukosa maji.
Akizungumza na waandishi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing’ataki ameeleza hatua kwa hatua kuhusu hali ya mto huo ambapo amefafanua ni mto ambao unafanya hifadhi iweze kuwa na vivutio vingi kwa maana wakati wa kiangazi kama hiki wanyama wengi wakubwa na wadogo wanafika kwa ajili ya kupata maji.
“Lakini kwa wanyama wanaishi kwenye maji hasa mamba, viboko na samaki wanaishi katika mto huu,kwa sasa hali ya mto huu Ruaha ni ngumu sana kwasababu hali ya maji ni mbaya, takribani sasa siku 80 huu mto hautiririshi maji yake , mto umeacha kutiririsha maji yake na maeneo machache yaliyobaki ni maeneo yenye madimbwi ambako kuna maji ambayo yanatumiwa na wanyama wote wanaofika katika maeneo haya
“Ni maeneo ambayo machache sana yamebaki katika mto huu na ukitizama kwa karibu maeneo haya maji yaliyoko kwenye haya madimbwi hata rangi yake imebadilika sio maji ya kawaida kwa maana ni maji machafu kwasababu wanyama wengi wanatumia na wanatumia katika maeneo haya wanaishi humo humo, wengine wanafia humo humo, wanajisaidia humo humo , wengine wanakuja wanakanyaga kwa hiyo maji ni machafu kwa ujumla.
“Maji haya sio mazuri kwa uhai wa wanyama lakini hawana namna , haya maeneo ndio machache yaliyobaki kwa hiyo wanyama wanakusanyika katika maeneo haya kwa ajili ya kupata maji. Uhai wa hifadhi hii kama nilivyosema unategemea uwepo wa mto Ruaha na hasa maji yake yanayotiririka kutoka kwenye bonde kubwa la Usangu ambalo liko ndani ya hifadhi ya taifa ya Ruaha.
“Tunatakribani kilometa 164 za mto huu ambao unapita ndani ya hifadhi ya mto huu wa Ruaha , baada ya kupita ndani ya hifadhi basi mto huu hutiririsha maji yake katika bwawa la Mtera , Kidato na Bwawa la Mwalimu Nyerere.Ni mto muhimu sana lakini sasa tunapozungumzia umuhimu wake na hali halisi sasa ilivyo ambapo maji hakuna kabisa hata tone, utabaini changamoto kubwa ya kimazingira kwa maana ya wanyama wanapata shida ya maji safi ya kunywa,”amesema.
Ameongeza lakini pia mazingira ya hifadhi yanaharibika kwa maana ya wanyama wanapokusanyika eneo dogo wanatumia kile kilichopo kwa kufuata maji kwenye madimbwi hayo, hivyo kuleta uharibifu mkubwa wa mazingira ndani ya hifadhi tofauti na kama maji yangekuwa mengi wanyama wangekunywa na kuendelea na shughuli zao.
“Kwa hiyo ukitizama au ukitembelea kando kando ya Mto Ruaha kwa sasa uoto wa asili sasa umeanza kuharibika kutokana na wanyama kuja kwa idadi kubwa katika eneo hili.Tumeona madhara mengine kwamba baadhi ya wanyama wakati mwingine hasa jamii ya samaki wamekuwa wanakufa kutokana na maji yaliyopo yanakuwa ni machafu na hali ya hewa pia hapa ni ya joto kipindi hiki.
“Hivyo maji yanapata joto lakini kutokana na ule uchafu na ukweli kwamba wanyama jamii ya samaki wanahitaji hewa nzuri ya kuvuta kwa maana ya Oxgen inapungua maji yanapokuwa machafu na kunakuwa na joto kwa hiyo wakati mwingine samaki wengi wanakufa katika kipindi hiki.
“Tulipofanya uchunguzi kwenye madimbwi haya tulichobani samaki wanakufa kwasababu ya kukosa hewa ya Oxgen ambayo inafanya waishi kwenye maji lakini pia tumeona katika kipindi hiki wanyama wanatafuta maeneo mengine ya kupata maji ya kutumia na wanatoka nje ya hifadhi na tunajua huko nao wanasababisha migogoro kati ya binadamu katika maeneo hasa kwa kuharibu mazao na mali nyingine,”amesema.
Ole Meing’ataki amesema kuwa madhara mengine yanayotokea ni wananchi kudhuru wanyama , miaka ya nyuma walikuwa wanaona magonjwa.Wanyama wakinywa maji kwenye madimbwi hayo basi vile vimelea vya magonjwa husambaa kwa urahisi, jambo lingine ambalo walikuwa wakiliona huko nyuma ni majangiri ambao walikuwa wanaingia katika baadhi ya maeneo ya hifadhi wanaweza kufika kwenye maeneo yenye maji na madimbwi kama haya na kuweka mitego yao na kuwanasa wanyama lakini pia wakati mwingine wanaweza kutumia sumu inayoweza kuua wanyama mbalimbali.
“Wanyama ambao wanakula mizoga na wanyama wengine ambao wanawakamata, tumeona wakati mwingine wakifanikiwa kufanya hivyo wanaondoka na nyama na hizo nyama zinakwenda kuuzwa kwa wananchi kitu ambacho ni cha hatari sana kwa usalama wa afya zao.
“Kwa hiyo huu Mto Mkuu Ruaha naweza kusema ni muhimu ni muhimu kwa mtazamo huo kwamba kweli ni kivutio kwasababu maliasili ambazo tunazo wanyamapori wakubwa na wadogo wanapatikana katika maeneo haya na ukiangalia utalii unaofanyika katika hifadhi kwa kiasi kikubwa kuna njia nyingi za utalii ambazo zinakwenda kando kando ya huu mto Ruaha kwasababu wageni wanaweza kuona wanyama kwa karibu.
“Kinachotokea katika huu mto ambao unaanzia katika bonde la Usangu tunaona kuna shughuli nyingi za kibinadamu ambazo tunazungumzia shughuli ambazo ni haribifu, ukataji miti ambao unafanyika , uchomaji moto ambao tunauona lakini uingizaji wa mifugo mingi katika eneo lile vyanzo vya maji kama tulivyoona limekuwa tatizo kubwa ambalo linasababisha maji kuisha , kilimo holela kinachofanyika ambacho maji yanapatikana hata kama yamepungua lakini yanatumika kwenye kilimo lakini siku ya mwisho maji haya hayarudi kwenye mkondo asili kwa maana kwenye mto.”
Aidha amesema wanaona kuna uchepushaji mkubwa wa maji katika maeneo mbalimbali ambapo unakuta baadhi ya wananchi wameanzisha mashamba na hawajali kwamba haya maji yanahitajika kwenye matumizi ya maliasili kama hizi za wanyama pori lakini pia kwa ajili ya uzalishaji umeme na matumizi mengine ya kiuchumi hasa kupitia eneo hilo.
“Tunafahamu maji yanapojaa kwenye bonde la Usangu hutiririka kupitia Mto Ruaha mkuu na ukipita basi hifadhi tunanufaika kupitia nafasi hii mazingira yatakuwa mazuri na tutapata idadi kubwa ya wageni wanaotembelea hifadhi kwasababu tunarasilimali hii ambayo imehifadhiwa na inategemea huu mto.
“Lakini huu mto unapotoka nje ya hifadhi ndio sasa huko maji yanakwenda maeneo mengine ambako kuna jamii ambazo zinatumia maji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tunazungumzia kilimo, tunazungumzia uvuvi , mathalani kama maeneo ya Mtera tunaona uvuvi unafanyika na maeneo mengine lakini maji haya baada ya kuzalisha umeme pale Mtera huelekea Kidatu mpaka Bwawa la Nyerere na huko njiani maeneo ambayo mto unapita kuna matumizi mengi mengi kwa hiyo tunapotumia maji vibaya kwenye bonde la Usangu tunafanya huu mto ruaha uendelee kuwa katika hali mbaya na ile nafasi ya mchango wake katika maeneo ya kiuchumi,
“Uhifadhi wa baianoai na matumizi mengine ya binadamu na uzalishaji umeme tunakosa hiyo nafasi kubwa sana , kwa hiyo madhara ya kuupoteza huu mto au kukauka ni makubwa sana sio tu kwa hifadhi kama tunavyoona utalii unaweza kuathirika lakini na huko maeneo mengine ambayo maji haya yanatumika,”amesema Ole Meing’ataki.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing’ataki akionesha hali halisi ya Mto Ruaha Mkuu ulivyokauka.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-RUAHA.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing’ataki akionesha hali halisi ya Mto Ruaha Mkuu ulivyokauka .
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing’ataki akisalimiana na baadhi ya Watalii waliokuwa wakipita katika daraja la mto Ruaha ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha,mkoani Iringa
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Godwell Ole Meing’ataki akiwa amesimama kwenye daraja la Mto Ruaha Mkuu ndani ya hifadi akionesha sehemu ndogo ya maji yaliyobaki,ambayo nao ni machafu hayafai kwa matumizi ya baadhi ya Wanyama.
0 comments:
Post a Comment