*****************
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Wizara ya Afya imeendesha mafunzo kwa Maafisa Afya 100 wa Mkoa wa Dar es Salaam kwaajili ya ufuatiliaji wa tetesi au washukiwa ambao wametoka katika nchi ambazo zinamaambukizi ya Ebola.
Akizungumza katika Mafunzo hayo leo Novemba 12,2022 Jijini Dar es Salaam Mtaalamu wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt.Biseko Palapala amesema mafunzo hayo ni kuwaweka wataalamu utayari endapo ikatokea mlipuko wawe na uwezo wa kufuatilia wale wote ambao watashukiwa ambao ni wasafiri watakaoingia nchini wakiwa na maambukizi ya virusi vya Ebola.
"Tunawapa ili kuwajengea uwezo kwasababu siku zote ugonjwa unatakiwa utambulike mapema pamoja na kutambua yule ambaye alikuwa na dalili za ugonjwa amekutana na watu gani ili kusudi wale watu wafuatiliwe kupunguza usambazaji wa ugonjwa". Amesema Dkt.Palapala.
Amesema Tanzania ni moja ya nchi ambazo ipo katika hatari ya kupatikana na maambukizi ya Ebola kwasababu inapakana na nchi ya Uganda ambayo tayari virusi vimeshaeneo nchini humo.
Aidha amesema Tanzania na Uganda ni nchi ambazo zinamuingiliano hivyo ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa lazima wafuatilie wale ambao wamekutana na yule mtu ambaye anamaambukizi.
Amesema mafunzo ni ya siku tano ambapo siku tatu za mwanzoni watakuwa wanatoa mafunzokwa maafisa afya lakini pia siku mbili watakuwa wanafundisha wale ambao watahusika na jamii moja kwa moja.
Amesema mafunzo hayo pia yanaendelea kutolewa katika mikoa mingine ikiwemo mkoa wa Kagera ili kusudi wataalamu waliopo kwenye mikoa mingine waweze kupatiwa uwezo ili kupambana na maambukizi ya Ebola.
Kwa upande wake Afisa Afya wa Jiji la Dar es Salaam, Bi.Siriel Killeo Amesema "mafunzo haya yamenijengea uwezo na utayari wa kuweza kufuatilia endapo kutakuwa na tatizo lolote la Ebola nchini kwasababu bila ya kuwa na utayari wakati janga likitokea inakuwa ni shida".
Nae Afisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw.Ally Kasembe amesema fursa waliyoipata wataenda kuitumia vizuri katika utekelezaji kwani elimu ambayo wamepatiwa ni bora na huenda ikaleta faida kubwa hapo baadae kwa maana haifahamiki kama maambukizi hayo yanaweza kuingia nchini ama la, hivyo tahadhari ni muhimu.
0 comments:
Post a Comment