Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akizungumza kwenye ufunguzi wa mbio za Marathon kuelekea uchaguzi Mkuu ngazi ya UVCCM unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2022 Jijini Dodoma.
Na Dotto Kwilasa,DODOMA
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson amewataka vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kutumia nafasi zao kubishana kwa hoja na kuendelea kudumisha amani ,umoja na mshikamano hali itakayosaidia kuwalinda Viongozi wa taifa .
Dkt.Tulia ameyasema hayo Jijini Dodoma leo Novemba 26,2022 wakati akifungua mbio za Marathon za vijana wa UVCCM katika viwanja vya Jamhuri katika kuelekea uchaguzi Mkuu wa UVCCM ngazi ya Taifa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2022 Jijini Dodoma .
Amesema ni jukumu la vijana hao kuacha malumbano na kubishana kwa hoja zinazojenga na kuongeza kuwa ikiwa vijana hao wataenzi amani na mshikamano itawasaidia kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya na kuwa na ari ya kufanya kazi kwa bidii .
Spika Tulia amesema,"Hakikisheni katika chaguzi zenu mnaenzi amani kama ilivyo itikadi ya Chama chetu ,msianzishe vioja vinavyolenga kubomoa bali hoja zitakazoeleza maendeleo yanayofanywa na Serikali na si vinginevyo".
Pamoja na hayo ameeleza kuwa vijana hao wana jukumu kubwa la kuwalinda viongozi wao kwa hoja zinazoeleweka ikiwa ni pamoja na kuelekeza mambo mengi yanayofanywa na Serikali.
"Msikae kimya,tangazeni miradi tuliyonayo achaneni kabisa na masuala yanayowapotezea muda ambayo hayajengi,kuna wakati mnasubiri mtu atoe hoja ili muanzishe kuleta vioja vyenu naomba muache hiyo tabia kwani sio utamaduni wa Chama chetu ,"amesema
Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuwapongeza vijana wa hamasa wa Chama hicho kwa juhudi zao
katika kuamsha ari kwenye matukio ya Viongozi wakuu na kueleza kuwa huo ndio uzalendo unaotakiwa kwa Kila kijana.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi ( UVCCM )Kenani Kihongosi amemshukuru spika Tulia kwa kukubali kuungana nao katika mbio hizo zilizoambatana na matembezi ya amani na kueleza kuwa hiyo ni fursa ya vijana kujenga Afya na kuepuka magonjwa.
0 comments:
Post a Comment