Timu ya Wataalamu kutoka Mamlaka Zinazohusika na Utoaji wa Vibali vya Kazi na Ukazi Kwa Raia Wa Kigeni Wanaokuja Kufanya Kazi Katika Miradi Mbalimbali Nchini Wakitembezwa Katika Mitambo ya Kuchakata Gesi Asilia Iliyopo Madimba Mkoani Mtwara. Wengine Katika Picha ni Wataalamu kutoka GASCO, Wataalamu Kutoka PURA, Wataalamu Kutoka NEEC na Taasisi ya UONGOZI.
Sehemu ya Wataalamu kutoka Ofisi Zinazohusika na Utoaji wa Vibali Vya Kazi na Ukazi Wakipatiwa Maelezo Kutoka kwa Meneja wa Kitalu cha Mnazi Bay kutoka kampuni ya Maurel and Prom, Bw. Laurent Jars mara baada ya Timu hiyo Kufika Eneo Hilo kwa Ziara ya Kikazi.
Wataalamu kutoka Ofisi Zinazohusika na Utoaji wa Vibali Vya Kazi na Ukazi Wakipatiwa Maelezo Kutoka kwa Mtaalamu kutoka Kiwanda cha Saruji cha Dangote kuhusu miundombinu ya kujaza gesi asilia kwenye magari inayomilikiwa na Kiwanda hicho
**********************
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imefanikisha ziara maalum kwa mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya kazi na ukazi kwa raia wa kigeni wanaokuja nchini kufanya kazi katika miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya mafuta na gesi asilia.
Ziara hiyo iliyofanyika hivi karibuni ililenga kuzijengea uelewa mamlaka husika kuhusu shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
Mamlaka hizo ni Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Idara ya Uhamiaji).
Ziara ilihusisha kutembelea miundombinu ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia iliyopo eneo la Mnazi Bay Mtwara inayoendeshwa na kampuni ya Maurel and Prom na mitambo ya kuchakata gesi asilia inayoendeshwa na GASCO (kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania - TPDC) iliyopo eneo la Madimba Mtwara.
Ziara pia ilihusisha kutembelea miundombinu ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia na kituo cha kujaza gesi asilia kwenye magari kinachomilikiwa na Kiwanda cha Saruji cha Dangote pamoja na mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani katika eneo la Bandari - Mtwara, mradi uliotekelezwa na unaoendeshwa na GASCO.
Akizungumza mara baada ya ziara, mjumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Suleiman R. Seng'enge alisema kuwa ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa kuwa imeongeza wigo wa uelewa kuhusu masuala ya mafuta na gesi, jambo ambalo litasaidia wakati wa kuchakata maombi ya vibali kwa raia wa kigeni wanaotaka kufanya kazi katika miradi ya mafuta na gesi asilia nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau, Bw. Charles Nyangi alisema kuwa, ziara hiyo itasadia katika utekelezaji wa matakwa ya kisheria ya ushiriki wa watanzania katika shughuli za mafuta na gesi asilia nchini.
Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, wakandarasi wanaotekeleza miradi ya mafuta na gesi asilia nchini wanapaswa kutoa kipaumbele cha ajira kwa watanzania kabla ya kuajiri raia wa kigeni. Aidha, Sheria hiyo pia inataka wakandarasi hao kutoa kipaumbele kwa huduma na bidhaa zinazopatikana nchini kabla ya kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Miongoni mwa majukumu ya PURA kwa mujibu wa Sheria hiyo ni kusimamia masuala ya ushiriki wa watanzania katika shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchni.
0 comments:
Post a Comment