Wednesday, 16 November 2022

WAZIRI MKENDA NA WAZIRI LELA MOHAMED WAONGOZA KIKAO CHA MAPITIO YA SERA NA MITAALA JIJINI DODOMA

...
 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prf .Adolf Mkenda (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed Hadid .
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  Lela Mohamed .


Na Mathias Canal, WEST-Dodoma.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prf Adolf Mkenda (Mb) pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed wameongoza Kikao cha kazi cha mapitio ya Sera na Mitaala.


Akizungumza katika kikao hicho cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na timu za mapitio ya Sera na Mitaala ya Elimu katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi-Ndejengwa Jijini Dodoma leo tarehe 15 Novemba 2022, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknoojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa mapitio hayo yanahusisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwa na mtazamo wa pamoja katika sekta ya elimu.


Waziri Mkenda amesema kuwa hatua za awali zimekamilika hivyo kwa sasa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inajiandaa kwa ajili ya kumpitisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan katika hatua zote zilizofikiwa kabla ya mkutano mkuu wa wadau wote wa sekta ya elimu kujadili mustakabali wa elimu ya Tanzania.


Waziri Mkenda amesema kuwa kabla ya mkutano wa wadau wa elimu nchini pia kutakuwa na mkutano wa kazi wa baraza la Mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara zote ili kujadili kwa kina kuhusu mustakabali wa sekta ya elimu na mapendekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu sekta ya elimu nchini.


Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Lela Mohamed amempongeza Waziri Mkenda kwa usimamizi madhubuti wa timu zote za mapitio ya sera na mitaala kwani imeonyesha nia ya dhati na umakini wa serikali katika kuhakikisha maboresho ya elimu yanakuwa shirikishi.


Amesema kuwa kazi hiyo ya Mapitio ya Sera na Mitaala yanafanyia kwa upande wa Tanzania Bara pamoja na Tanzania Visiwani-Zanzibar kwa lengo la kuimarisha elimu kwa pande zote mbili za Muungano ili wanafunzi wanapokutana chuo kikuu wawe na uelewa wa pamoja.


"Sisi Mawaziri tumepewa maagizo ya kuhakikisha tunasimamia mabadiliko haya ya sera na mitaala bila kupishana, hata kama wale wanakuwa wakiogelea kule baharini na hawa wanakulia kwenye milima na kwenye madini lakini mwisho wa siku yule mvuvi na yule muwindaji wawe katika lugha moja katika mifumo yetu" Amesisitiza Mhe Lela


Kadhalika, Waziri Lela amepongeza kwa wadau kutoka pande zote mbili za muungano kushirikishwa katika mapitio ya sera na mitaala kwani mjadala huo pia unasaidia kamati ya Zanzibar katika utekelezaji wa majukumu yake.


Amesema kuwa mpaka sasa maoni yote yanayokusanywa bado ni mali ya Wizara kabla ya mapendekezo ya serikali kwa ujumla ambayo inaongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan pamoja na Mhe Dkt Hussein Mwinyi kwa upande wa Zanzibar ambaye tayari ameridhia kupitishwa katika hatuazili zofikiwa.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger