



















(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
*******************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KUPITIA Mradi wa HEET, Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) kinatarajia kutumia zaidi ya shilingi Bilioni kumi na saba kwaajili ya kuendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo, kujenga majengo na miundombinu mingine mipya na kusomesha wanataaluma katika ngazi ya uzamili na uzamivu kwenye Vyuo Vikuu mbalimbali duniani.
Ameyasema hayo leo Novemba 26,2022 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Balozi Mwanaidi Maajar katika Mahafali ya 15 ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) yaliyofanyika chuoni hapo.
Amesema Baraza linaendelea kuiomba Serikali na wafadhili wengine kusaidia kuongeza miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji chuonii hapo kwani kumekuwa na changamoto za maabara na vifaa vingine muhimu vya kufundishia na kujifunzia.
"Neema ya ongezeko la wanafunzi kila mwaka imekuwa haiendi sambamba na ongezeko la miundombinu kama vile kumbi za mihadhara, upungufu mkubwa wa hosteli kwa wanafunzi na gharama kubwa ya kusomesha wanataaluma katika ngazi ya uzamili na uzamivu". Amesema
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Prof.William Anangisye ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa rasilimali muhimu zinazohitajika katika uendeshaji wa Chuo.
Amesema Serikali imeendelea kujenga na kuboresha miundombinu muhimu na kutoa fedha za uendeshaji wa Chuo kwa ujumla. Ambapo pia amewashukuru wabia wao wa kitaifa na kimataifa waliochangia gharama za uandaaji na uendeshaji wa programu mbalimbali za masomo ambazo wahitimu wameshiriki na kunufaika nazo.
Kwa upande wake Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Prof.Stephen Maluka amesema kwa mwaka 2022/2023 Chuo kimetenga shilingi 480,035,000/= kwaajili ya mafunzo ya watumishi ambapo kati ya kisi hicho, shilingi 101,448,00/= ni kwaajili ya mafunzo ya muda mfupi na shilingi 378,587,000/= kwa ajili ya mafunzo ya muda mrefu.
Ameeleza kuwa jumla ya watumishi 54 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
"Chuo kimetenga dola za Kimarekani 1,000,000 sawa na Bilioni 2.3 za Kitanzania kwaajili ya mafunzo ya muda mrefu ya watumishi kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ambapo jumla ya watumishi 16 wanasomeshwa Digirii za Umahiri na Uzamivu katika Vyuo mbalimbali duniani". Amesema Prof.Maluka.
0 comments:
Post a Comment