Serikali yabaini watumishi hewa 1855 nchini
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mheshimiwa George Simbachawene amewataka wakuu wa mikoa ambayo imekutwa
na watumishi hewa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi waliohusika
kulipa na kupokea mishahara hewa.
Akizungumza na wakuu hao wa mikoa mara baada ya kukabidhiwa ripoti hizo,
Waziri Simbachawene aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa
wanawakamata watumishi hao kwa makosa waliyobainika nayo na hatua
stahiki.
"Wananchi wanataka kusikia hawa waliokuwa wanaiibia serikali
wamechukuliwa hatua gani mara baada ya kutangazwa badala ya kuishia
kuwatangaza kuwa ni watumishi hewa na wanalipwa mishahara," alisema.
Jumla ya watumishi hewa 1855 wamebainika kuwepo katika mikoa mbalimbali
nchini huku mkoa wa Mwanza ukiwa na watumishi hewa 334, Arusha 270 na
Sungida 202.
Mikoa ya Mwanza, Arusha na Singida inaongoza kwa kuwa na watumishi hewa wengi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kutoka kwa wakuu wa mikoa, watumishi
waliobainika kuwa ni hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara ni walimu
na madaktari ambao ni marehemu na wastaafu.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais John Magufuli, kuwaagiza
wakuu hao wa mikoa kuwasilisha ripoti ya watumishi hewa ambayo
waliikabidhi kwa Simbachawene jana jijini Dar es Salaam kabla ya
kuiwasilisha kwa Waziri wa Utumishi na kujumilisha na ripoti za sekta
zote nchini na hatimaye kumfikishia Rais.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema jumla ya watumishi hewa 334
walibainika kwenye mkoa huo hususani katika Halmashauri ya jiji la
Mwanza ambalo lina watumishi hewa 72 pekee.
Katika mkoa wa Arusha jumla ya watumishi hewa 270 walibainika katika
kipindi cha wiki mbili na kusababisha upotevu wa Sh. bilioni 1.188 kwa
mwezi March pekee.
Katika mkoa wa Singida jumla ya watumishi hewa 202 walibainika na mkoa
wa Kigoma wenye watumishi hewa 171 ambao wamesababisha hasara ya Sh.
milioni 114.6 kwa mwezi.
Mikoa mingine ni Kilimanjaro wenye jumla ya watumishi hewa 111 ambao
waliolipwa Sh. milioni 281.4 kwa mwezi mmoja na Dodoma watumishi hewa
101 waliolipwa Sh. bilioni 297 kwa muda wa miezi sita.
Pia katika mkoa wa Morogoro watumishi hewa waliobainika ni 122 ambao
walilipwa Sh. milioni 450.79 kwa mwezi March pekee na mkoa wa Mara
watumishi hewa 94 ambao walilipwa Sh. milioni 121.1 kwa mwezi mmoja.
Mkoa wa Mbeya ambao umeungana na mkoa mpya wa Songwe ulibainika kuwa na
watumishi hewa 98 ambao walilipwa mishahara kiasi cha Sh. milioni 459.6.
Katika jiji la Dar es Salaam watumishi hewa waliobainika ni 73 ambao wamelipwa Sh. milioni 379 kwa mwezi mmoja.
Mikoa mingine ni mkoa wa Pwani uliobainika kuwa na watumishi hewa 150,
Ruvuma watumishi hewa 37 ambao walilipwa Sh. milioni 58. 4, Njombe
watumishi hewa 34 ambao walilipwa Sh. Milioni 20.107 na mkoa wa Rukwa
wenye watumishi hewa 18 waliolipwa mishahara Sh. Milioni 55.64.
Watumishi wengine hewa walibainika katika mikoa ya Simiyu 33 ambao
walilipwa Sh. Milioni 320.993 , Tabora jumla ya watumishi hewa 48 ambao
walilipwa Sh. Milioni 118, Tanga watumishi hewa 24 na Lindi watumishi 57
waliolipwa Sh. Milioni 36.
Mikoa mingine ni Katavi wenye watumishi hewa 21 ambao walilipwa Sh.
milioni 120 kwa miezi sita, kagera 14 ambao walilipwa Sh. milioni 49.
147 kwa mwezi, Geita wenye watumishi hewa nane na Manyara wenye
watumishi hewa watano.
Aidha katika mkoa wa Shinyanga haukubainika kuwa na watumishi hewa
kutokana na malengo waliyokuwa wamejiwekea tangu mwaka 2014, ikiwamo
kukagua idadi ya watumishi walioko kazini na wanaotakiwa kulipwa
mishahara kila mwezi.
Pia katika ripoti hizo walibainika watumishi watoro ambao walikuwa
wakiendelea kulipwa mishahara licha ya kutokuwepo kazini kwa muda mrefu.
Katika mkoa wa Dodoma jumla ya watumishi watoro 38 walibainika, Iringa
145 na Kagera watumishi 248 ambao pia wanaendelea kuchunguzwa.
Mkoa wa Manyara jumla ya watumishi watoro 50, Mtwara watumishi 285
watoro, Mwanza watumishi watoro 205, Pwani watumishi watoro 50 , Rukwa
watumishi watoro 139 na Simiyu watumishi watoro 62.
Mkoa wa Singida watumishi watoro 29 na Tanga jumla ya watumishi watoro 502.
Watumishi hao watoro ni wale walioacha kazi lakini wamekuwa wakiendelea
kulipwa mishahara na wengine walio kwenye matatizo ya kiutumishi.
0 comments:
Post a Comment