Kumekuwa
na taarifa zinazoendelea kupotosha umma na baadhi ya vyombo vya Habari
kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokuwa ikitekeleza
majukumu yake tarehe 5 Aprili, 2016 ililitaka Jeshi la Polisi
kuwasilisha Mkataba ulioingiwa Kati ya Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi
Enterprises Ltd kuhusu mradi wa Utambuzi wa Alama za Vidole AFIS
(Automated Fingerprint Identification System).
Ofisi
ya Bunge inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili kwamba, taarifa
hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha umma kutokana na kile
kilicho amuliwa na kamati hiyo.
Ukweli
kuhusu jambo hili ni kwamba tarehe 5 Aprili, 2016, kamati hiyo
ilikutana na kujadili Taarifa ya Ukaguzi wa hesabu zilizokaguliwa za
fungu 28, Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2014
ambapo kamati pamoja na mambo mengine ilibaini dosari katika utekelezaji
wa mkataba huo.
Kutokana
na dosari hizo, kamati iliomba Afisa Masuhuli ambaye ni Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha maelezo ya kina kwa
maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge
ili kamati iweze kuchambua na kujadili maelezo hayo kabla ya kupendekeza
kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua.
Kufuatia
agizo hilo, kamati ilimwandikia pia Katibu wa Bunge taarifa kuhusu
agizo hilo tarehe 12 Aprili, 2016 ili kupatiwa maelezo hayo kutoka kwa
Afisa Masuhuli.
Aidha,
Ofisi ya Bunge ilimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani
tarehe 12 Aprili, 2016 kuwasilsha Taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya
Kamati Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotokana na kikao
hicho cha tarehe 5 Aprili 2016 kabla ya tarehe 18 Aprili, 2018 kama
ilivyoshauriwa na kamati .
Hivyo
ni vyema Umma ukafahamu kuwa kilichoombwa na Kamati ni Maelezo ya
utekelezaji wa Mkataba huo na sio Mkataba kama inavyoripotiwa na baadhi
ya vyombo vya Habari ambapo Ofisi ya Bunge iliomba maelezo hayo
yawasilishwe kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM 15 Aprili, 2016.
0 comments:
Post a Comment