Monday, 25 April 2016

MBOWE ATISHWA ZIGO

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
BARAZA la Mawaziri Kivuli la Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana lilikutana kwa saa kadhaa mjini Dodoma kujadiliana mambo mbalimbali, huku likimtwisha mzigo  
Kiongozi wao, Freeman Mbowe.
Moja ya ajenda kubwa iliyotawala kikao hicho  ni jinsi gani mawaziri vivuli hao watakavyokabiliana na mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli ndani ya Bunge kuhusiana na hoja nzito zitakazoibuka.
Mawaziri   vivuli wanatokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
Kikao hicho   kilifanyika kuanzia saa  8.00 mchana hadi 11:30 jioni huku  mawaziri vivuli hao wakijadili   mwenendo wa Bunge kwa sasa, maandalizi ya bajeti za Kambi ya Upinzani na wajibu wao.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya kikao hicho kiliiambia MTANZANIA kuwa  mawaziri wamemtaka Mbowe kusimama kidete na  kuhakikisha anasimama imara na kutoa kauli kuhusu mambo yanayoendelea ndani ya Bunge.
“Kikao chetu kilikuwa cha kawaida, tulikuwa tunakumbusha wajibu wetu kama mawaziri vivuli na mambo ya kusimamia ndani ya Bunge.
“Tumejadili kwa kina kuhusu mwenendo wa Bunge na namna waandishi wa wanavyopata shida kutimiza wajibu wao, tumemwomba Mbowe atoe msimamo wetu.
“Pia  suala la maandalizi ya bajeti yetu  tumeliangazia kwa kina, hasa upande wa kambi yetu na namna ya kujipanga zaidi… maana Bunge limekuwa kama kibogoyo.
“Serikali imekuwa inaliendesha, jambo hili linatisha,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Juhudi za kumpata Mbowe  kuzungumzia majukumu aliyopewa hazikuzaa matunda kwa vile kwa  muda mwingi  simu yake ya kiganjani haikuwa hewani.
Mwishoni wa wiki iliyopita, Mbowe  aligoma kuwasilisha maoni ya kambi  hiyo kuhusiana na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, huku akitaka maelezo ya muundo wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli akisema haujaundwa kihalali.
Alisema Rais Magufuli ameshindwa kutekeleza sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ya mwaka 1980  ambayo hutolewa katika gazeti la Serikali kila linapotaka kuundwa Baraza la Mawaziri.
Badala yake  kazi zimekuwa zikifanyika kwa maagizo, alisema.

Mbowe alisema mpaka sasa Serikali inafanya kazi bila kuwa na mwongozo wa utendaji kazi kwa wizara mbalimbali.
Alisema  hiyo  ina maana  Serikali inafanya kazi kwa kauli za Rais na mawaziri bila kufuata mwongozo wowote wenye msingi na uhalali wa  sheria, jambo ambalo Kambi ya Upinzani haiwezi kushiriki kwa vile ni  uvunjaji wa Katiba.
“Sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ya mwaka 1980, kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake.
“Mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali kwa kila wizara unaotumika ni ule uliochapishwa kwenye Gazeti la Serikali namba 494A la tarehe 17/12/2010.
“Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali hii kuendesha kazi zake kwa Mwongozo wa 2010 inamaanisha kwamba majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu bado ni yale yale yaliyochapishwa mwaka 2010, kwa sababu gazeti hilo la Serikali halijafutwa,” alisema Mbowe huku akishangiliwa na wabunge wa upinzani.
Akiwasilisha hoja ya pili, Mbowe  alisema kuna uvunjwaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusiana na bajeti unaofanywa na Serikali.
Alisema Bunge la Bajeti   kwa mujibu wa ibara ya 63(3)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepewa mamlaka ya kujadili  utekelezaji wa kila wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti kwa madhumuni ya kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Serikali.
Mbowe alisema ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutekeleza majukumu ya Serikali, kifungu cha 41(1) cha  Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015  kinaelekeza kwa Serikali itawasilisha bungeni kwa idhini, bajeti ya nyongeza ya fedha zilizotumika ambazo zimezidi kiwango kilichoidhinishwa na Bunge au kwa madhumuni ya kugharamia mahitaji ambayo hayakupangwa.
“Mheshimiwa Spika utaratibu huu unatiliwa nguvu na Sheria ya Fedha za Umma  wa mwaka 2001(Public Finacne Act, 2001) ambako kifungu cha 18 (3) na (4) kinaitaka Serikali kuleta Bungeni bajeti ya nyongeza (mini-budget) kwa ajili ya kupata idhini ya Bunge ikiwa fedha zilizoidhinishwa awali hazikutosha.
“Utaratibu huo wa  sheria  umekuwa ukivunjwa na Serikali kwa  kufanya matumizi ya fedha ambazo hazikuidhinishwa na Bunge jambo ambalo linaua dhana ya madaraka ya Bunge ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

“Ili kuthibitisha jambo hilo, kwa mfano, bajeti ya maendeleo iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2015/16  ilikuwa ni Sh  bilioni 883.8 na katika   fedha hizo,  fedha za ndani zilikuwa ni Sh bilioni 191.6,” alisema.
Alisema jambo la kushangaza hadi kufikia Machi mwaka huu, wizara hiyo ilikuwa imepokea kutoka Hazina Sh bilioni  607.4 kama fedha za ndani.
Source: Mtanzania
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger