Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, inayoongozwa na Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya Ukawa imeanza kazi kwa staili ya aina yake baada ya kutangaza neema ya bima ya afya kwa wananchi wa Manispaa hiyo.
Imeahidi
kuanzisha mpango maalum ambao kila mwananchi wa Manispaa hiyo
atachangia Sh. 40,000 kwa mwaka ili aunganishwe na mpango wa matibabu wa
bima ya afya ambao utawawezesha kupata matibabu ya bure katika
hospitali mbalimbali.
Mpango
huo utaanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu, huku bajeti ya Manispaa
hiyo ikiongezeka kwa asilimia 59 kutokana na kukua kwa mapato ya ndani.
Wazee
wa Manispaa hiyo nao wametangaziwa neema ya matibabu bure kwani
watapewa kadi maalum zitakazowawezesha kutibiwa hospitali za umma.
Mapato
hayo yametokana na ukusanyaji madhubuti katika kodi za majengo,
mabango, leseni za biashara, huduma za kuegesha magari, hoteli na ruzuku
ya serikali kuu.
Bajeti
ya mwaka 2016/2017 katika Manispaa hiyo inafikia Sh. Bilioni 248.47
ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ambayo ilikuwa ya Sh. Bilioni
156.24.
Katika bajeti ya mwaka huu kuna ongezeko la Sh. zaidi ya bilioni 92.
Meya
wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob aliwasilisha bajeti hiyo jana
jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani.
Baada
ya kuwasilisha bajeti hiyo, Madiwani wote wakiwamo wa upinzani na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) waliipitisha kwa kauli moja ili ianze kuwahudumia
wananchi.
Akisoma
bajeti hiyo, Jacob alitaja ukusanyaji wa mapato ya ndani umeingiza Sh.
bilioni 64.28 na kwamba imeongezeka kutoka Sh. bilioni 56.6 za mwaka
jana.
Licha
ya bajeti ya mwaka huu kulenga kugharamia huduma za matibabu, lakini
imelenga kujenga shule ya bweni katika Kata ya Goba kwa gharama ya Sh.
milioni 250, ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule, kujenga vyumba vya
madarasa na ununuzi wa madawati 30,000.
Kazi
nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa Barabara kuelekea kituo
cha daladala cha ya Simu 2000 na Barabara ya Akachube ambazo
zimetengewa Sh. bilioni 50.
Kuhusu suala la usafi, Meya Jacob alisema kila Kata itakuwa na gari lake la kuzolea takataka na Manipaa imetenga Sh. 2.2b .
Manispaa hiyo ina jumla ya Kata 25 na Sh. bilioni 3.6 zimetengwa kwa ajili ya gharama za kusafirisha takataka.
Aidha,
katika bajeti hiyo, Manispaa inatarajia kununua Trekta lenye kijiko kwa
ajili ya kutengeneza barabara na zimetengwa Sh. bilioni 1 kwa ajili ya
kazi hiyo.
Kazi
nyingine za fedha hizo ni kuweka sakafu ngumu katika masoko yote ya
manispaa, ili kuondoa adha ya uchafu na matope katika msimu wa mvua na
zimetengwa Sh. bilioni 1.65.
Kuhusu vijana na wanawake Manispaa hiyo imetenga Sh. bilioni 4.7 kwa ajili ya kuwakopesha na kila Kata itapata Sh. milioni 200.
0 comments:
Post a Comment