Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetishia kuichukulia Kenya hatua
kali isiposalimisha kwa mahakama hiyo washukiwa watatu wanaokabiliwa na
mashtaka ya kutatiza mashahidi.
Msemaji wa ICC Fadi el Abdallah
alisema mahakama hiyo itairipoti Kenya kwa Baraza la Mataifa Wanachama
wa Mkataba wa Roma (ASP) kama itaendelea kushikilia msimamo wa kutowawasilisha Wakenya hao watatu mbele ya mahakama hiyo
mjini Hague, Uholanzi.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Bi Fatou
Bensouda, amepata kibali cha kuwakamata aliyekuwa mwanahabari Walter
Osapiri Barasa, wakili Paul Gicheru na Philip Bett kwa madai ya kutatiza
mashahidi katika kesi dhidi ya Naibu Rais William Ruto na mwanahabari
Joshua arap Sang.
Agizo la kukamatwa kwa Bw Barasa lilitolewa
Oktoba 2013 ilhali lile la kukamatwa kwa Philip Bett na Paul Gicheru
lilitolewa Septemba 2015 kwa madai kuwa walihonga mashahidi.
Kesi
dhidi ya Bw Ruto na Sang ilitupiliwa mbali mapema mwezi huu kwa misingi
kuwa ilikosa ushahidi wa kutosha kutokana na mashahidi kutatizwa.
Akihutubia
hafla ya maombi mjini Nakuru mnamo Jumamosi, Rais Kenyatta alitangaza
kuwa hakuna Mkenya mwingine atakayefikishwa katika mahakama ya ICC
kujibu mashtaka.
Alisema kusitishwa kwa kesi hizo ndio mwisho wa ushirikiano baina ya Kenya na mahakama hiyo ya kimataifa.
“Ukurasa
huo tayari tumefunga na hatutakubali Mkenya kurudi katika mahakama ya
ICC. Tuna mahakama zetu za kutatua matatizo yetu,” akasema rais katika
uwanja wa michezo wa Afraha.
“Kenya ikipuuza agizo la
kuwasilisha washukiwa hao, majaji watawasilisha ripoti yao mbele ya
Baraza la Mataifa Wanachama wa Mkataba wa Roma ambalo litachukua hatua
zinazostahili,” akasema Bw Fadi.
Kifungu cha 87(7) cha Mkataba
wa Roma kinasema: “Nchi mwanachama ikikataa kushirikiana na ICC na
kutatiza utendakazi wake, mahakama inaweza kuwasilisha malalamishi kwa
baraza la ASP.”
Wiki iliyopita, Bi Bensouda alisema
kusambaratika kwa kesi dhidi ya Bw Ruto na Bw Sang kulichangiwa kwa
kiwango kikubwa na kutatizwa kwa mashahidi na akataka washukiwa hao
watatu wapelekwe ICC.
Alisema mashahidi 17 ambao walikuwa wameandaliwa na upande wa mashtaka walijiondoa baada ya kutishwa na kutengwa.
Hapo
jana, Fadi alisema ICC inajua kuhusu tangazo la Rais Kenyatta wa Kenya
kutosalimisha washukiwa hao na kuwa inafuatilia hatua hiyo kwa karibu.
0 comments:
Post a Comment