Hatima ya mkataba tata wa kampuni ya Lugumi Enterprises ipo mikononi
mwa Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya jana, Kamati ya Bunge ya Hesabu
za Serikali (PAC) kuwasilisha muhtasari wa ilichokibaini baada ya
kupitia maelezo ya utekelezaji wake.
Moja kati ya mambo yaliyomo
katika muhtasari huo ni kulitaka Bunge kutoa ruhusa kwa kamati ndogo
iliyoundwa na PAC juzi kuchunguza kwa kina mkataba huo wa kufunga mtambo
wa utambuzi wa vidole (AFIS), ikiwa ni pamoja na kutembelea vituo
vinavyodaiwa kufungwa mashine hizo.
Kamati ya PAC ilinusa
ufisadi kwenye mkataba huo wa AFIS ulioitaka Lugumi kufunga mitambo
kwenye vituo vya polisi 108 kwa gharama ya Sh37 bilioni lakini
ilibainika kwamba kampuni hiyo ililipwa kiasi cha Sh34 bilioni zaidi ya
asilimia 90 ya fedha zote ilhali imefunga mashine 14 tu mkoani Dar es
Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema jana muda
mfupi baada ya kukutana na Spika kuwa wamepeleka mapendekezo hayo na
wanachokisubiri ni kauli ya ofisi yake.
Muhtasari huo umekuja
siku moja baada ya PAC kuwaweka kitimoto Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Meja Jenerali Projest Rwegasira na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi,
Abdulrahman Kaniki kuhusu mkataba huo.
Bunge liliagiza maelezo ya kina
kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo baada ya kubaini kuwa una
maswali mengi kuliko majibu na liliwaita viongozi hao ili kupata
ufafanuzi wa kina.
Katika maelezo yake jana, Aeshi alisema kesho
watakuwa wameshapata majibu kutoka Ofisi ya Spika na wataweka wazi
mambo yote waliyokuwa wakiyajadili kuhusu Lugumi.
“Hili ni jambo
zito ambalo linahusu usalama kwa hiyo ni lazima twende nalo taratibu
ili kujua ukweli na kuja na majibu ya kueleweka... kila kitu tutawaeleza
Jumamosi,” alisema.
0 comments:
Post a Comment