Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda ameagiza kufanyika kwa uchunguzi jengo la Machinga Complex
kubaini uhalali wa mkataba uliowezesha ujenzi wa jengo hilo, ikiwa ni
pamoja na gharama halisi za ujenzi.
Alisema hayo kutokana na jengo hilo kuwa na deni la zaidi ya Sh bilioni 36, kiasi ambacho ni mara tatu ya thamani halisi ya jengo hilo na kuleta shaka ya ufisadi ndani yake. Jengo hilo lina thamani ya Sh bilioni 12.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa itaanza kufanya uchambuzi wa mkataba ili kupata uhalali wa gharama na kujua kiwango kinachostahili kulipwa na wafanyabiashara hao.
“Katika miradi mingi duniani huu ni wa aina yake, mradi ambao kabla haujaanza unaweka jiwe la msingi unaanza kudaiwa benki, mpaka unakuja kumaliza deni lako ni kubwa linakaribia robo mbili au tatu ya mkopo wenyewe, kabla hata hujaanza kupangisha hata mtu.
“Kwa takwimu zinaonesha tumekopeshwa na jengo limejengwa Sh bilioni 12.7, lakini mpaka dakika hii mnadaiwa Sh bilioni 36 na nyinyi ndio mnatakiwa kuzilipa, sasa kwa maelezo hayo ndio mnapata picha kwa nini tumeamua kujipa muda,” alisema Makonda.
Alisema katika maelezo ya awali yanaonesha kuwa jengo hilo lina mkanganyiko mkubwa na inawezekana kuwa ni miongoni mwa miradi iliyofanyiwa ufisadi mkubwa.
Hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene aliifuta bodi inayosimamia jengo hilo na kumsimamisha kazi meneja anayesimamia jengo hilo na kumtaka kwenda katika ofisi za jiji kwa ajili ya kumpangia kazi nyingine.
Katika hatua nyingine, Simbachawene alilikabidhi jengo hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa mpango wa kuwaingiza wafanyabiashara bila masharti huku ukiangaliwa utaratibu mpya kwa wafanyabiashara hao.
0 comments:
Post a Comment