Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema idadi ya watumishi hewa katika wilaya hiyo, imeongezeka hadi kufikia 89 wakiwa wamesababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja.
Aidha,
Hapi amebaini uwepo wa watumishi vivuli 81 katika kada ya ualimu na
hivyo kutoa siku saba kwa maofisa utumishi wa wilaya hiyo, kuhakiki
watumishi vivuli ili kubaini idadi yao na hasara waliyosababisha.
Hapi
aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake jijini Dar es Salaam, na kueleza kuwa awali wakati akiingia katika
ofisi yake wiki iliyopita alikuta kuna watumishi hewa 34 waliokuwa
wamesababisha hasara ya Sh milioni 512.
Alisema
baada ya kufanya uhakiki zaidi walibainika watumishi hewa wengine 55
walioisababishia serikali hasara ya Sh milioni 619 na hivyo kufanya
jumla ya hasara kuwa Sh 1,131,754,081.
“Bado
uhakiki wa kina unaendelea ili kuhakikisha tunamaliza hili tatizo la
watumishi hewa katika wilaya ya Kinondoni, awali walikuwa 34 lakini sasa
wameongezeka 55 na kufikia 89,” alisema Hapi.
Akifafanua
kuhusu watumishi vivuli, Hapi alisema watumishi hao ni wale ambao
walihamishwa bila kufuata taratibu na hivyo kuendelea kupokea mshahara
wa kazi yake ya awali badala ya kazi yake mpya.
Alisema
walibaini kuwepo kwa walimu katika idara ya elimu ya msingi 42 ambao
baada ya kufuatilia hawakuonekana katika shule yoyote ya wilaya hiyo.
“Kwa
hiyo hili nalo ni tatizo kuna walimu wengine wanapokea mshahara mkubwa,
lakini mtu alishahamishwa lakini anaendelea kupokea mshahara wa zamani
ambao haufanyii kazi,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Hapi aliwataka wafanyabiashara ndogo ndogo walioko
katika maeneo yasiyoruhusiwa kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa baada
ya siku saba alizotoa kukamilika.
Alisema
agizo hilo alilitoa ikiwa ni sehemu ya kuweka Manispaa ya Kinondoni
katika hali ya usafi ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais John Magufuli
ya usafi wa kudumu.
0 comments:
Post a Comment