MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki ametaka kufanyika msako
wa kuwabaini, kuwakamata na kuchukulia hatua kali za kisheria watu
wanaokatisha wanafunzi masomo kwa kuwapa mimba.
Pia Sadiki amesema serikali haitasita
kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu wakuu wa shule za msingi na
sekondari, ambao ni hodari kutaja wanafunzi wenye ujauzito bila kuwataja
wahusika au hatua zinazochukuliwa kukomesha vitendo hivyo.
Akizungumza na walimu wa shule za msingi, sekondari, watendaji wa ngazi zote za Halmashauri ya Wilaya ya Same, mkuu wa mkoa alitaka wasichana walindwe ili kutimiza ndoto zao.
“Mkuu wa wilaya hakikisha wanaume hao wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola, ni aibu nasikia wengine ni viongozi, walimu… mnaharibu maisha ya watoto wetu bure, mkubali msikubali watoto wa kike ndiyo wanaongoza kufanya vizuri katika mitihani, angalia kidato cha nne na sita,” alisema Sadiki.
Alisema ni jambo la ajabu kwa walimu kwa kushirikiana na waratibu elimu kata kutofuatilia mienendo ya wanafunzi wanaporejea nyumbani, na kutaka taarifa iandaliwe kwa ajili ya hatua zaidi.
0 comments:
Post a Comment