Siku moja baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Tanesco, William Mhando, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), inaandaa utaratibu wa kukata rufaa dhidi ya hukumu
hiyo.
Aprili 14, mwaka huu Mahakama hiyo ilimwachia huru Mhando na
wenzake wanne akiwamo mkewe, Eva na maofisa watatu wa Tanesco; Francis
Mchalange, Sophia Misida na Naftali Kisinga waliokuwa wakikabiliwa na
mashtaka ya matumizi mabaya ya fedha.
Mashtaka mengine yaliyokuwa
yakiwakabili ni kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za
Serikali.
Hata hivyo, washtakiwa hao waliibwaga Takukuru baada ya
mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma
hizo.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema,
Hakimu Hellen Riwa alisema kwa mujibu wa ushahidi, suala la msingi
lilikuwa ni mkataba kati ya kampuni ya Santa Clara Supply Limited na
Tanesco.
Alisema katika mkataba, Mhando alikuwa mshtakiwa wa kwanza,
akituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kutangaza
masilahi yake kwa kampuni ya Santa Clara inayomilikiwa na Eva ambaye ni
mkewe.
“Suala la msingi ni kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo alihusika
katika utoaji wa zabuni na nani aliyekuwa na uamuzi wa mwisho,” alisema.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Tunu Mley
ilisema imefikia uamuzi huo baada ya wadau wengi kuhitaji kujua hatua
zitakazochukuliwa na chombo hicho baada ya hukumu hiyo.
“Takukuru
inawataka wadau na wananchi kwa ujumla kutambua kwamba ni utaratibu wa
kisheria kwamba upande mmoja usioridhika na hukumu iliyotolewa kukata
rufaa katika mahakama ya juu,” ilieleza taarifa hiyo.
Baada ya hukumu
hiyo juzi, Wakili wa Takukuru, Leonard Swai aliomba Mahakama kuingilia
kati.
0 comments:
Post a Comment