Waziri Simbachawene Azipongeza Halmashauri 10
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhe.George Simbachawene amezipongeza halmashauri 10 zilizofanya vizuri
katika vigezo vya kutoa takwimu kwa usahihi, kupanga walimu katika shule
zenye upungufu na kutuma ruzuku shuleni kwa wakati.
Aidha Waziri Simbachawene aliwataka wasimamizi wa mpango huo ambao
umewekwa na serikali kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu nchini
wahakikishe kuwa wanautekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu ili uweze
kufanikisha malengo yaliyo kusudiwa.
Akizungumza kwenye hafla maalum iliyoandaliwa na Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa ajili ya kutoa motisha kwa halmashauri
kumi bora zilizofanya vizuri Mhe.Simbachawene aliwataka viongozi wa
Halmashauri 10 zilizofanya vizuri pamoja na halmashauri ambazo
hazikufanya vizuri katika vigezo vilivyowekwa kujituma na kuhakikisha
wanafanya kazi kwa ubunifu ili kuleta tija katika elimu nchini.
Aliongeza kuwa kuwa taifa linapaswa kujenga misingi imara ya elimu ya
awali ili kuwa na wahitimu wa elimu ya juu ambao wameandaliwa vizuri na
wanaoweza kukabiliana na changamoto za ajira za sasa.
Aliwataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa utakaoleta
mabadiliko katika utoaji huduma na kufanya kazi kwa matokeo na
kutekeleza malengo waliyojiwekea kwa wakati na kuzingatia viashiria
vilivyoanishwa na kuvitekeleza ipasavyo.
Aidha, aliwakumbusha umuhimu wa kuweka takwimu na kutumia fedha
zitakazoletwa kwa mujibu wa taratibu za serikali kwani huo ndio msingi
wa kuleta tija katika maeneo yao ya kazi.
Halmashauri 10 kati ya 181 zilizopo nchini ambazo zimefanya vizuri
katika vigezo vilivyowekwa na serikali ni halmashauri za Mbinga, Nkasi,
Chato, Busega, Lushoto, Liwale, Sikonge, Mbarali, Halmashauri ya Wilaya
ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya ya Tabora.
0 comments:
Post a Comment