Sunday 17 September 2023

GST YATAKIWA KUWA KINARA WA TAARIFA ZA MADINI NA HUDUMA BORA ZA MAABARA

...


Kupitia utekelezaji wa muelekeo mpya ujulikanao kama Vision 2030, Serikali yaweka mkakati wa kuifanya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) kuwa kinara wa upatikanaji na utoaji wa taarifa za madini na pia huduma bora za maabara.

Hayo yamesemwa leo tarehe 17 Septemba, 2023 Mkoani Morogoro na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde alipokuwa akifunga kikao kazi cha Menejimenti ya GST ambacho kilikuwa mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa maagizo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan wakati akizungumza na wakuu wa Taasisi za umma Jijini Arusha na kupitia muelekeo mpya wa Wizara wa VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri


"Nchi yetu imegawanywa katika QDS 322, ambapo QDS moja ina eneo la kilometa za mraba 2916. Ni asilimia 16 pekee ya eneo lote nchini ndilo limefanyiwa utafiti wa jiofizikia kwa teknolojia ya kisasa ya kurusha ndege yaani High Resolution Airborne Geophysical Survey.

Sote tunaona kwamba iwapo tukiweza kufanya utafiti wa eneo hata kwa asilimia 50 tu, namna ambavyo sekta ya madini inakwenda kulinufaisha Taifa letu kwa kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa uchumi.

Mh. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan , ameonesha dhamira ya dhati ya kuikuza sekta ya madini ili iongeze mchango zaidi kwenye Pato la Taifa la Nchi yetu.

Taasisi hii inategemewa kwa taarifa za awali za muelekeo wa miamba, hivyo tunakwenda kuifanya kuwa kinara wa taarifa na takwimu za madini nchini,sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wake ili kukidhi mahitaji ya dunia ya leo na pia kuimarisha maabara yake kwa vifaa vya kisasa”Alisema Mavunde.

Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, Afisa Mtendaji Mkuu wa GST, Dkt. Mussa Budeba alieleza kuwa kikao kazi hicho ni matokeo ya Mkutano wa Mhe. Rais alipokutana na Wenyeviti na Watendaji wa Taasisi za Serikali ambapo alielekeza Taasisi zijiwekee mikakati ya kujiendesha kwa tija na faida na kupunguza utegemezi kutoka Serikalini.

Vilevile, mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga alibainisha kwamba pamoja na masuala mengine kikao kazi hicho kililenga pia kuongeza ari ya kazi, ushirikiano baina ya watumishi kwa kufanya kazi kwenye Timu ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mh. Rebecca Nsemwa alishukuru kwa GST kuchagua kufanyia kikao Morogoro na kuiomba GST kuuweka Mkoa wa Morogoro kwenye mkakati wao kwani wanao utajiri mkubwa wa madini.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger