WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda,akiangalia Kompyuta kabla ya kuzikabidhi kwa wakuu wa vyuo wakati wa hafla ya ugawaji Kompyuta kwa vyuo vya ualimu awamu ya tatu ambapo jumla ya Kompyuta 300 zimetolewa
Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog-DODOMA.
WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikina na Serikali ya Canada imedhamiria kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo vya Ualimu ili kuongeza ubora wa elimu ,pamoja na kuwa na miundombinu rafiki kwa wanafunzi na walimu.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji Kompyuta kwa vyuo vya ualimu awamu ya tatu ambapo jumla ya Kompyuta 300 zimetolewa kupitia ufadhili wa Mradi wa kuendeleza Elimu ya Ualimu nchini (Teacher Education Support Project -TESP) unaogharimu Dola za Canada milioni 53.
Amesema kupitia mradi huo,mazingira ya kufundishia yataboreshwa ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kujifunzia katika Vyuo vya Ualimu ili kuongeza ubora wa elimu ,pamoja na kuwa na miundombinu rafiki kwa wanafunzi na walimu hali itakayosaidia kuwepo ufaulu mzuri na kuzalisha walimu wenye ari ya kuendeleza vipaji vyao kwa vizazi vingine.
Amefafanua kuwa jumla ya vyuo 13 vimepata Kompyuta 50 ambapo ,Vyuo 4 kati ya hivyo vimepata Kompyuta 30 na Vyuo 9 Kompyuta 20 na kwamba Vyuo vyote 35 vitapatiwa Kompyuta Mpakato moja kwa ajili ya kusaidia idara zingine vyuoni.
“Leo mtapatiwa Kompyuta za Mezani na Kompyuta Mpakato na Mgao wa kompyuta hizi umezingatia uwiano kati ya wanachuo na vifaa vilivyopo katika Vyuo vyetu kwa sasa,”amesema.
Waziri Mkenda amevitaja Vyuo hivyo vya Ualimu vilivyopatiwa Kompyuta kuwa ni pamoja na Marangu,Kleruu,Vikindu,Patandi,Korogwe,Mpwapwa,Shinyanga,Ilonga,Tarime,Tandala,Butimba,Mtwara na Morogoro.
Amesema dhima ya Vyuo vya Ualimu nchini ni kuandaa walimu mahiri na wanaotosheleza mahitaji katika shule za Awali, Msingi na Sekondari.
“Kutokana na dhima hiyo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika Vyuo vyote vya Ualimu vya Serikali nchini mkazo ukitolewa katika uboreshaji wa miundombinu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na matumizi ya TEHAMA kama nyenzo muhimu katika ufundishaji na ujifunzaji,"amesema.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa Uboreshaji huo utakwenda sawa na maendeleo makubwa katika matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika ufundishaji na Ujifunzaji.
Kadhalika amesema Wizara itaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Vyuo mbalimbali nchini ikiwemo ukamilishaji wa Chuo cha Kabanga, Ujenzi wa vyuo vipya vya Sumbawanga, Dakawa, Mhonda na Ngorongoro unaendelea na kwamba ukarabati na ujenzi wa baadhi ya miundombinu katika vyuo vya Morogoro, Mpwapwa, Tukuyu, Kasulu, Butimba na Patandi nao unaendeleana huku ukitarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2021/2022.
"Lengo letu ni moja nalo ni kuongeza thamani ya elimu nchini jambo tunalofanya kwa vitendo ambapo hadi sasa Wizara imetoa mafunzo ya matumizi ya Tehama katika kufundishia na kujifunzia kwa wakufunzi wote 2,300 kutoka Vyuo vya Ualimu vya Serikali yote 35,hali hii itasaidia kupunguza uwiano wa matumizi ya kompyuta kwa Wanachuo kutoka Wanachuo 28 kwa Kompyuta moja hadi kufikia Wanachuo 2 kwa Kompyuta 1 vyuoni,”amesema.
Katika hatua nyingine Prof. Mkenda amewaagiza wakuu wa vyuo hao kutunza Kompyuta hizo ambapo amesema zimenunuliwa kwa gharama kubwa hivyo kila Mkuu wa Chuo kuhakikisha kuwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji vyuoni.
Naye,Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Omari Kipanga amesema licha ya juhudi zilizopo katika maboresho ya elimu, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu nchini hivyo kunahitajika jitihada ili kuzaliwa walimu wengine wengi kupitia vyuo hivyo.
“Kila mwaka ni lazima tuzalishe walimu wa kutosha,Serikali ni kweli imewekeza ila bado kuna changamoto ya walimu bila walimu hatuwezi kutoka nyinyi ni chemchem ila tunaenda kubadilisha mitaala tutaangalia haya masuala ya teknolojia,”amesema.
Kwa upande wake,Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Prof. Caroline Nombo amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada ambapo amedai mchango wa Canada katika mradi huo ni jumla ya Dola za Canada milioni 53.
Amesema mchango wa Serikali ya Tanzania ni katika kugharamia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa vyuo ikiwemo gharama za malipo ya chakula kwa wanachuo na mafunzo ya ualimu kwa vitendo.
Prof.Nombo amesema dhumuni kuu la mradi huo ni kuendeleza elimu ya ualimu,kwa kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji kupitia uboreshaji wa miundombinu ya utoaji wa mafunzo ya ualimu katika vyuo vya ualimu vya Serikali 35.
“Utoaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.Kuimarisha mifumo na miundombinu ya tehama.Kuwaendeleza kitaaluma na kuwajengea uwezo watendaji katika utoaji wa elimu ya ualimu,”amesema.
Amesema hadi kufikia Disemba mwaka 2021 jumla ya Dola za Canada milioni 42 sawa na asilimia 79.25 ya fedha zote za mkataba zilikuwa zimepokelewa kutoka kwa mfadhili wa mradi Globar Affars Canada hadi kufikia Disemba 2021 wastani wa utekelezaji wa malengo ya mradi ulikuwa ni asilimia 75.83.
0 comments:
Post a Comment