Friday, 4 February 2022

NIVISHE NISOME, MTAKA WASHIRIKIANA KUCHOCHEA ELIMU DODOMA

...

 

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 Blog-DODOMA.

TAASISI ya 'Nivishe Nisome' inayojihusisha na masuala ya elimu nchini, imetoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi 241 katika shule ya Msingi Mbabala,Kata ya Mbabala,mkoani hapa huku wakitarajia kutoa sare za shule 5000 katika shule zote za Mkoa wa Dodoma ili kuchochea elimu.

Hayo yamejiri leo Mkoani hapa wakati wa ziara ya Taasisi hiyo katika shule ya Msingi Mbabala ikiongozana na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma kwa lengo la kuhamasisha elimu kwa watoto na kuwapa moyo wa kuendelea kutamani kusoma na kujifunza zaidi.


Akizungumzia ujio wa ziara yao, Mkurugenzi wa Nivishe Nisome,Godfrey Kilimwomeshi,amesema wao kama taasisi ya vijana wanaojihusisha na uchechemzi wa elimu nchini, wanatamani kuona kila kijana anasoma katika mazingira mazuri na kuhakikisha  wanatumia jitihada zao zote kuwapatia sare  wanafunzi wasiojiweza.

Amesema ,maono ya Taasisi hiyo ni kuwajali wanafunzi wasiojiweza hususani wale wa  pembezoni jambo litakalowafanya wasahau shida zao japo kwa muda na kujiona bora kama wenzao na kwamba hali hiyo itasaidia kuboresha na kuinua kiwango cha elimu yao.

"Tunatambua haki ya kila mtoto ni elimu,tunaamini hapa kwenye elimu ndio wanatoka viongozi mbalimbali na ndio maana "Nivishe Nisome'" tumekuwa na maono ya kuwajali wanafunzi  kadiri tunavyojaaliwa ,"ameeleza Mkurugenzi huyo na kuongeza;

"Tunaamini mtoto akiwa katika mzingira mazuri basi na uelewa wake unakuwa mkubwa tofauti na akiwa kwenye mazingira",amesisitiza.

Kutokana na hayo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Anthony Mtaka ameishukuru Taasisi hiyo kwa mchango wake katika elimu huku akiwataka wazazi na walezi wa watoto hao waliopewa sare za shule kuwahimiza masomo watoto wao ili wasome kwa bidii .

Pia ametoa angalizo kwa walimu wa shule hiyo kuwahimiza  wazazi wote wenye watoto wa  madarasa ya mitihani ya Taifa kuwapa muda wa kujisomea na kuwapunguzia kazi za kufanya nyumbani ili watoto wasome na wawe na nia na mahangaiko moyoni hali itakayo ongeza ufaulu.

"Kupitia msaada huu wa sare za shule,sisi kama Wazazi tunapaswa tusimame kwenye nafasi yetu na si kujibweteka,wenzetu hawa wa Nivishe nisome wamekuja kwangu wakasema sisi hatuna uwezo wa kujenga shule lakini tunataka kutoa sare kwa shule 5000 hii inahamasisha wanafunzi kwenda shule,na kusoma Kwa bidii",amesema Mtaka.

Mtaka ambaye ameambatana na Taasisi hiyo shuleni hapo ameonesha pia kukerwa na tabia ya baadhi ya watoto ambao wapo kwenye rika la kuwepo shuleni lakini wanaishia kuzurura ovyo mitaani kwa madai ya kutafuta vibarua  masokoni na minadani wakati wa masomo na kusema hataki kuona mtoto yoyote mwenye umri huo  akiwa mtaani.

"Malezi ya watoto ni ya jamii nzima,ukiona mtoto  wa mwezio hayupo darasani wakati wa masomo hakikisha unamrudisha darasani,hayo ndiyo malezi mema,na sio kumtumikisha mtoto wa mwenzako muda wa masomo,ni dhambi kubwa,"amesema Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma huku akiongeza kuwa;

Watoto wote ni mali ya serikali ndio maana kila wakati huwa nasisitiza sitaki kuona mwanafunzi anazurura mtaani wala mnadani,kila mzazi mwenye mtoto aliyefikia umri wa kuanza darasa la kwanza apelekwe shule na mzazi asipompeleka mtoto shule akamatwe akafanye kazi za usafi shuleni,"amesema. 

Katika hatua nyingine,Mtaka amewataka Afisa Elimu Sekondari na Afisa Elimu Msingi wa jiji la Dodoma kutoa maagizo kwa Wakuu wa shule zote kuwa wakati wa kufunga shule wazazi wa wanafunzi wawe wanapewa taarifa mapema ili wawepo shuleni kwa ajili ya kubadilishana changamoto za watoto wao  na kuona namna ya kusaidia na walimu kuzitatua.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Nathaniel Mwijumbe ameahidi kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kushukuru kwa msaada huo na kusema  utawasaidia wanafunzi kuwa na moyo wa  kujifunza na wenzao.

Amesema baadhi ya wanafunzi hushindwa kuwa na ufaulu mzuri kwenye masomo Kutokana na upweke unaotokana na umasikini hivyo kupitia msaada huo wa sare za shule wengi wao watajiona hawako peke yao kwani nyuma yao kuna watu wanaowajali na kuwalinda.

"Sisi kama viongozi tupo na wewe katika juhudi zako za kupeleka mbele elimu,tutahakikisha watoto wanasoma vizuri kwa kufanya jitihada ikiwa ni pamoja na kuwapatia wanafunzi  chakula shuleni,hii itaongeza ufaulu mara dufu na hapo tutakuwa tumetimiza ndoto yako ya kuondoa ziro katika Mkoa wa Dodoma,"amesisitiza Mwl.Mwijumbe. 

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger