WANAFUNZI wanaosoma katika shule mbili za msingi za Kijichi wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, wako hatarini kuathirika kiafya na kimaadili kutokana na madarasa yao kutumika kama sehemu ya kuvuta bangi.
Vitendo hivyo vimefichuliwa juzi na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Kijichi waliotembelea shule hizo kwa ajili ya kutoa misaada kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu katika kuadhimiasha miaka 45 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Kijichi B, Stephano Cherehani, alisema matumizi ya dawa hizo za kulevya tayari yameonekana kuwa na athari katika maendeleo ya elimu kutokana na baadhi ya wanafunzi kupata madhara.
Alisema watu wanaoingia shuleni huko kila siku kwa nia ya kuangalia michezo ya mpira wa miguu, hutumia madarasa kuvuta bangi na kuacha mabaki kila mahali.
Cherehani alisema wakati mwingine watu hao wanavuta nje ya madarasa hayo kipindi cha asubuhi, jambo ambalo linaleta usumbufu kwa wanafunzi wanapotaka kuingia darasani kuanza vipindi vya masomo.
“Jambo hili linatuathiri sisi walimu na wanafunzi pia, uvutaji wa bangi umekuwa kama jambo la kawaida, lakini chanzo kikubwa ni huu uwanja wa mpira ambao unatumika na jamii muda wote,” alisema.
Aliomba serikali kuingilia kati kwa kudhibiti vitendo hivyo ili kuwaweka wanafunzi katika hali ya utulivu na kukidhi matakwa ya mazingira bora ya ujifunzaji na ufundishaji.
“Wanafunzi hawawezi kusoma kwa umakini kama kuna mabaki ya bangi au mtu anavuta nje ya darasa, tunaomba watu hawa wadhibitiwe haraka,” alisema.
Katibu wa Wazazi wa CCM katika kata hiyo, Magdalena Komba, alimhakikishia mwalimu mkuu huyo kuwa watalifanyia kazi haraka kwa kwenda kuripoti katika vyombo husika ili eneo hilo liwe salama kwa utoaji wa elimu kwa watoto.
“Pamoja na kwamba leo (juzi) tumekuja kuwasaidia watoto wetu wanaoishi katika mazingira magumu, lakini suala hili la uvutaji bangi holela limenigusa na nitakwenda kuwasiliana na vyombo husika ili kulikomesha,” aliahidi.
Komba pia alisema jumuiya hiyo ni sawa na kiranja katika malezi ya watoto na ndio maana katika maadhimisho hayo, wameamua kutoa misaada ya sare za shule na madaftari kwa wanafunzi 27 wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Mwanafunzi Hamisi Shamte aliyenufaika na msaada huo, aliishukuru jumuiya hiyo kwa kuwatambua na kisha kuwapa msaada huo ambao utawasaidia katika safari yao ya elimu.
Diwani wa Kijichi, Athuman Nyamlani, aliahidi kuliwasilisha suala hilo kwenye vyombo vya dola ili wanaojihusisha na vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.
0 comments:
Post a Comment