Wananchi wakishuka kutoka katika kivuko cha MV Kazi ambacho kilileta hitilafu hivi karibuni. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala (katikati) akimsikiliza Mhandisi wa Tehama Magogoni feli Jijini Dar es Salaam Bw.Omary Mayila mara baada ya kutembelea na kuangalia maendeleo ya kivuko cha MV Kazi ambacho kilileta hitilafu hivi karibuni. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kivuko Magogoni Feli Mhandisi Jamal Waziri.Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala (kulia) akizungumza na fundi wa vivuko magogoni Feli Bw.Benard Kaluse mara baada ya kutembelea na kuangalia maendeleo ya kivuko cha MV Kazi ambacho kilileta hitilafu hivi karibuni.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
*************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala ametembelea na kuangalia maendeleo ya Kivuko cha MV Kazi ambacho kilileta hitilafu kwa siku nzima ya tarehe 04/02/2022.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuona maendeleo ya Kivuko hicho Bw.Kilahala amesema kulitokea hitilafu ya msuguano chini na kuonekana kuingiza maji kwenye kivuko hivyo wakaamua kukisitisha kufanya kazi kwa usalama zaidi na kukifanyia marekebisho.
Aidha Bw.Kilahala amesema tayari kivuko hicho kimeshatengenezwa na kimerudi kuendelea kutoa huduma hivyo amewaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza kwa siku hiyo.
"TEMESA tumejipanga kuhakikisha wakati wote matengenezo yanafanyika katika vivuko vyote nchini, tuna mafundi wakutosha pia kuna kikosi maalumu cha kuhudumia vivuko hivi". Amesema Bw.Kilahala.
Amesema Serikali imeshatenga fedha za kutosha kuhakikisha vivuko vyote vinafanyiwa matengenezo makubwa na kwa wakati na hivi karibuni kivuko cha MV Kazi kitafanyiwa marekebisho makubwa kuhakikisha hakitaleta usumbufu katika utoaji huduma.
Pamoja na hayo amesema ununuzi wa kivuko cha nne tayari umeshaingia kwenye bajeti ya mwakani kwahiyo kuanzia mwezi Julai wataanza kutengeneza kivuko hicho, hivyo changamoto zitokanazo na vivuko hivyo utaenda kupungua kwa kiasi kikubwa pale watakapoongeza kivuko cha nne.
Kwa upande wa abiria wanaotumia vivuko hivyo wameipongeza Serikali kundelea kuwajari wananchi hasa wanaovuka katika vivuko vilivyopo feli magogoni kwani pindi vivuko vikiwa na hitilafu kidogo mara nyingi hufanya jitihada za haraka kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya vivuko kwa haraka na kwa wakati.
0 comments:
Post a Comment