Tuesday 4 January 2022

Naibu Waziri Ummy Aeleza Mikakati Ya Serikali Ya Kuboresha Mazingira Ya Watu Wenye Ulemavu

...


NA. MWANDISHI WETU
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vyuo ili kuendelea kutatua changamoto wanazokutana nazo.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Dkt.  Khalid Salum Mohamed alipomtembelea ofisini kwake Januari 03, 2022 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kujionea shughuli za watu wenye ulemavu katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Naibu Ummy alibainisha kuwa, tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi za kitanzania billion 8 kwa lengo ujenzi wa vyuo vya watu wenye ulemavu na ukarabati wa majengo chakavu ya kundi hilo nchini.

“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanazingatiwa ambapo ametoa shilingi bilioni 8 kwa ajili Ujenzi wa vyuo vipya viwili na ukarabati wa vyuo sita vya watu wenye ulemavu ili waweze kupata ujuzi kupitia elimu watakayopata na kuyafikia malengo yao”.alisisitiza Naibu Waziri Ummy

Aidha mikakati mingini ni pamoja na kuendelea kutoa vifaa saidizi kwa watu wenye mahitaji maalumu pamoja na kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki katika maeneo yanayowazunguka ili kuwapa nafasi ya kushiri vyema katika shughuli zao za kila siku.

“Serikali itaendelea kutenga bajeti ya kutosha, kuwawezesha vifaa saidizi, kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuendana na hali zao pamoja na kuhakikisha haki na usawa kwa watu wenye ulemavu vinapewa kipaumbele kwa kuzingatia sheria ya watu wenye ulemavu Namba 9 ya Mwaka 2010,”alisema

Hata hivyo naibu Waziri Ummy alimhakikishia Dkt. Salim kuwa wataendelea kudumisha ushirikiano baina yao kwa lengo la kuendeleza jitihada za kuwahumia watu wenye ulemavu nchini.

“Watu wenye ulemavu waliopo Zanzibar na Bara ni kitu kimoja hata mazingira ya changamoto zao zinawiana ni vyema kuitumia fursa ya kuendelea kuzitatua changamoto hizo huku tukidumisha ushirikino,”alisisitiza

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi (SMZ) Dkt.  Khalid Salum Mohamed alieleza kuwa, wamendelea kuratibu masuala ya watu wenye ulemavu ikiwemo uwezeshwaji kiuchumi, upatikanaji wa elimu jumuishi pamoja na kuwajengea uwezo ili kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.

“Kipekee nikupongeze kutenga muda wako kufika Zanzibar hii ni faraja kwa kuzingatia umuhimu wa masuala yanayowahusu watu weye ulemavu, tutaendelea kuboresha mshikamano ya kiutendaji baina yetu ili kuunga mkono juhudi za viongozi wetu,”alisema Dkt. Khalid


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger