Na Dinna Maningo, Tarime
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Valentine Maganga amesema kuwa watu wa wilaya ya Tarime ni majasiri si waoga na hawana aibu kumkosoa mtu.
Akizungumza na Malunde 1 blog Katibu huyo alisema kuwa wananchi wa Tarime wako tayari kumkosoa mtu yeyote na hawana mambo ya kona kona kwa kuwa ukosoaji kwao ni utamaduni.
"Tarime siyo ya mchezo ni wilaya ya kuwapima viongozi ukiletwa Tarime ujue kuna kupanda cheo au kushushwa,watu wake ni majasiri hawana aibu, kukukosoa kwao ni jambo la kawaida ni watu wasio na kona kona ukikosea hawaogopi kusema kwa sababu ndiyo utamaduni wao" amesema Maganga.
Maganga amewaomba viongozi wa Chama na Serikali walioko Tarime kushirikiana katika maendeleo na kutatua changamato zinazowakabili wananchi kwakuwa hitaji kubwa la wananchi ni kusikilizwa na kutatuliwa kero zao.
Wakizungumza na Malunde 1 blog kwa nyakati tofauti,Baadhi ya wananchi wameunga mkono kauli hiyo,Mwita Ryoba mkazi wa kijiji cha Matongo-Nyamomgo anasema kuwa wilaya hiyo hutizamwa kama mahali pa kuwapima viongozi utendaji wao wa kazi.
"Tarime ndiyo kipimo cha viongozi maana sisi watu wa Tarime hatuna uoga wala kumvumilia kiongozi anayekwenda kinyume tunapenda haki na hatupendi uonevu na tuna ujasiri ambao unatusaidia kutoogopa kumkosoa mtu yeyote hata kama ni kiongozi wakurya ndiyo tuko hivyo hata akija mgeni akiishi Tarime naye anakuwa jasiri", anasema Ryoba.
John Mseti mkazi wa kijiji cha Turugeti kata ya Bumera anasema" Tarime ni kipimo cha matendo ya watu hasa viongozi tumeshuhudia baadhi walioletwa kufanya kazi Tarime wakashushwa vyeo na wengine kuondolewa kwenye nafasi za kazi"
"Wapo waliokuwa DC Tarime walitumbuliwa ,wapo walioletwa kuwa RPC wamepanda kutoka kuongoza wilaya mbili za kipolisi Tarime/Rorya sasa wanaongoza mikoa,wapo waliokuwa OCD hapa Tarime leo ni RPC,wapo watendaji waliokuwa nafasi za kawaida na wamepanda vyeo huko Serikalini na kwenye vyama" anasema Mseti .
Chacha Marwa mkazi wa mtaa wa Sabasaba anasema kuwa watu wa Tarime si wakorofi kama inavyodhaniwa bali ni watu wanaojiamini,wenye msimamo,wanapenda haki na hawapendi kuonewa.
Rhobi Marwa mkazi wa Rebu anasema kuwa faida ya mtu kuwa jasiri inamsaidia kutokuwa na uoga katika kufanya maamuzi sahihi na kwamba kumkosoa mtu ni kumsaidia kujua tatizo lake ili ajisahihishe.
Muhiri Chacha Mkami mkazi wa kijiji cha Nyangoto kata ya Matongo anasema"Watu wa Tarime usiwaone hivyo ukija kama wewe ni kiongozi huwa hawana papara watatulia kwanza we utaona hawasemi jambo kumbe wanakupima kwanza matendo yako,siku wakikuamria hutoboi.
"Hata kwenye siasa ukipewa uongozi alafu ukaichezea nafasi uliyopewa kukubadilikia ni dakika moja ndiyo maana utaona Tarime inaongozwa na CCM na Chadema wao hawaangalii chama wanaangalia mtu atakayefaa bila kujali anatoka chama gani,ukifanya vizuri watakusema kwa mazuri ukifanya vibaya utasemwa kwa mabaya" anasema Muhiri.
Lucy John anasema kuwa watu wa Tarime ni wachapa kazi si tegemezi na ujituma kuhakikisha wanajiinua kiuchumi wakiwemo wanawake na hata uchumi ukiyumba hawakati tamaa kutafuta pesa.
0 comments:
Post a Comment