JESHI la Polisi wa Uholanzi wanasema wamempata mtu akiwa hai katika sehemu ya gurudumu la ndege iliyotua katika uwanja wa ndege wa Amsterdam wa Schiphol kutoka Afrika Kusini.
Safari za ndege kutoka Johannesburg hadi Amsterdam huchukua takriban saa 11, huku ndege ya mizigo ikiaminika kusimama mara moja, jijini Nairobi, Kenya.
Si jambo la kawaida sana kwa wanaopanda ndege kimagendo kuishi, kutokana na baridi na oksijeni kidogo kwenye miinuko ya juu. Umri na utaifa wa mwanaume huyo bado haujabainishwa, polisi wanasema.
“Mwanaume huyo alipatikana akiwa hai katika sehemu ya gurudumu upande wa pua ya ndege na alipelekwa hospitalini akiwa katika hali nzuri,” msemaji wa Polisi wa Kijeshi wa Uholanzi Joanna Helmonds aliambia shirika la habari la AFP.
“Inashangaza kwamba mtu huyo bado yuko hai,” alisema.
Kwa mujibu wa mtangazaji wa Uholanzi NOS, joto la mwili wa mtu huyo liliongezeka katika eneo la tukio na wakati gari la wagonjwa lilifika, aliweza kujibu maswali ya msingi.
Msemaji wa idara ya shehena ya mizigo Cargolux alithibitisha katika barua pepe kwa Reuters kwamba mtu huyo alikuwa kwenye ndege inayoendeshwa na Cargolux Italia.
Kulingana na data ya ndege, ndege pekee ya Cargolux ya mizigo kutoka Johannesburg hadi Schiphol Jumapili pia ilisimama Nairobi.
Haijulikani iwapo mwanaume huyo alipanda ndege hiyo nchini Afrika Kusini au Kenya.
0 comments:
Post a Comment