Sunday, 23 January 2022

Waziri Bashungwa: Wakandarasi Wazembe Kutopatiwa Kazi Za Tarura

...


Na. Angela Msimbira, Njombe
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff kuwaorodhesha makandarasi wote ambao wako kwenye rekodi ya kutokufanya vizuri na wababaishaji kufutwa na kutofanya kazi za TARURA nchi nzima.

Ameyasema hayo mapema leo wakati akikagua barabara ya Igosi –Ujindile-Wangama yenye urefu wa kilometa 16.9 iliyopo kata ya Wangama katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe ambayo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha changarawe kutokana na Fedha za Tozo ya Mafuta.

Waziri Bashungwa amesema kuwa Makandarasi ambao hawafanyi vizuri wasiwe wanahamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine, badala yake wapewe kazi makandarasi ambao wanauwezo wa kufanya kazi kwa viwango na kasi inayotakiwa.

“Serikali ya Awamu ya Sita inataka kupeleka huduma kwa wananchi kwa kuboresha mawasiliano ya miundombinu ya barabara hasa vijijini, Rais wetu anataka kuiboresha TARURA ili iweze kuhudumia watanzania, Makandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea hawahitajiki kwa sasa “, amesema Waziri Bashungwa

Waziri Bashungwa amesisitiza kuwa moja ya vitu ambavyo vitafanyika kwa Makampuni na Makandarasi wazembe na rekodi zinaonyesha ni wazembe ameelekeza apelekewe taarifa zao ili wasipatiwe kazi za TARURA kwani Serikali itafanya kazi na Makandarasi watakaofanya kazi kwa weledi na kukamilisha miradi kwa wakati na ameelekeza kuwepo kwa kanzidata kwa ajili ya Makampuni na Makandarasi ambayo yanafanya kazi vizuri ili waweze kupatiwa kazi za TARURA.

Amesisitiza kuwa lengo la kuanzishwa kwa TARURA nchini ni kuhakikisha inawasaidia wananchi wa vijijini katika Suala zima la ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuwasaidia watanzania ambao ni wakulima kuwafungulia fursa za kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi, hivyo ni wajibu kutumia makandarasi wanaofanya kazi kwa uaminifu na kuhakikisha miradi wanayopatiwa na Serikali inakamilika kwa wakati.

Akiwasilisha taarifa kuhusu ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Mhandisi Boniface Kasambo ameeleza kuwa barabara ya Igosi-Ujindile-Wangama ni muhimu kwa wanachi wa eneo hilo kwa kuwa inatumika kusafirisha mazao ya biashara ikiwemo parachichi, viazi na mbao kutoka mashambani Kata ya Wangama na Igosi kupeleka katika masoko ya Njombe Mji na Makambako kupitia barabara kuu ya Njombe -Makete.

Mhandisi Kasambo amesema ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuanza hivi karibuni, umeidhinishiwa zaidi ya shilingi milioni 400 na utajumuisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe, kuchimba mifereji na kujenga makalati.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger