Wadau kutoka sekta na Idara mbalimbali za Serikali wamekuta leo jijini Dar es Salaam kujadili rasimu ya mpango mkakati wa nne wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambao utatumika kwa miaka mitano hadi 2026. Katika kikao kazi hicho cha siku moja, wadau wamefurahishwa na jinsi ambavyo TEA imeweka vipaumbele katika mambo ya kimkakati ikiwemo TEHAMA.
Katika majadiliano hayo, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imepongezwa kutokana na jitihada zake za kusimamia na kuboresha miundombinu ya Elimu hasa katika mazingira ambayo ni magumu kufikika kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka TAMISEMI Bw. Musa Otieno ambaye alikuwa mmoja wa wadau katika kikao hicho amesema, TEA imefanya kazi nzuri sana ya kuboresha miundombinu ya shule ambapo imejenga madarasa, nyumba za waalimu, matundu ya vyoo, mabwalo ya vyakula pamoja na kununua madawati kwenye maeneo ya pembezoni mwa miji ambako ni ngumu kufikika.
Jitahada zote hizi zinalenga kusogeza huduma za sekta ya elimu karibu na wananchi ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kusoma karibu na mazingira anayoishi na hili linadhihirika wazi kwani mpango mkakati wa miaka mitano ijayo umebainisha kazi zinazooenda kufanyika katika kusimamia upatikanaji wa elimu bora, alisema Otieno
Nae mdau mwingine kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw.Gerald Sando, ameishukuru Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kazi zake na kusema kazi hizo ni endelevu na zinaonekana kwa macho.
Sando amesema, kazi za TEA zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kuongeza thamani kwenye maisha ya wale wa kipato cha chini kupitia mradi wa kuongeza ujuzi (SDF) ambao unafadhiliwa na TEA.
Kikao kazi cha kupitia rasimu ya mpango mkakati wa Mamalaka ya Elimu Tanzania (TEA) wa miaka mitano hadi 2026 kimefanyika jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Mkuu Bi. Bahati Geuzye.
Akitoa salaam za ukaribisho Mkurugenzi wa huduma za Taasisi Dr. Erasmus Kipesha ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho alisema, tangia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeanzishwa mwaka 2001, hii ni rasimu ya nne ya mpango mkakati.
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa lengo la kuongeza nguvu za Serikali katika kuinua upatikanaji wa elimu bora kwa usawa katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara na elimu ya juu kwa Tanzania Zanzibar.
Mkurugenzi wa huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha akitoa salaam za ukaribisho kwa wajumbe (hawapo pichani) waliohudhuria kikao kazi cha siku moja kujadili rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye akitoa hotuba ya ufunguzi katika kikao kazi cha siku moja cha kujadili rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA kwa wadau wa masuala ya elimu (hawapo pichani)
Baadhi ya wadau waliohudhuria kikao kazi cha siku moja wakifuatilia uwasilishwaji wa rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA.
Baadhi ya wadau waliohudhuria kikao kazi cha siku moja wakifuatilia uwasilishwaji wa rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA.
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI Bw. Musa Otieno akichangia maoni yake kuhusu rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA
Bw.Gerald Sando kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa – Dar es Salaam akitoa maoni yake kuhusu rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA.
Mkurugenzi wa huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt Erasmus Kipesha akiwasilisha rasimu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa TEA kwa wadau wa masuala ya elimu.
0 comments:
Post a Comment