Wednesday, 25 March 2020

MAHAKAMA YAJIPANGA KUKABILIANA NA CORONA.....KESI AMBAZO UPELELEZI HAUJAKAMILIKA HAZITAPOKELEWA

...

Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya nchini, wameagizwa kuzingatia maelekezo ya tangazo la serikali namba 296 la mwaka 2002 linaloeleza kesi zote zilizokamilika upelelezi zipokelewe mahakamani na kuanza kusikilizwa mara moja.

Kadhalika, kesi ambazo upelelezi wake haujakamilika wasizipokee wazingatie tangazo hilo kufuatia agizo la serikali kuzuia mkusanyiko kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, katika mkutano wake na waandishi wa habari, kuhusu mhimili huo unavyounga mkono juhudi za serikali.

"Imefika wakati sasa mahakimu wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya wafanye kazi kwa kuzingatia tangazo hilo na kama kesi upelelezi haujakamilika, basi ziishie hukohuko na si kupelekwa mahakamani kufuatia agizo la serikali kutoka kwa Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu," alisema Jaji Kiongozi.

Alisema mahakama imeongeza kasi ya matumizi ya mifumo hiyo kwa kanda ya Dar es Salaam kwa kesi zote za jinai zinazoahirishwa kutokana na sababu mbalimbali, watuhumiwa waliopo katika Gereza la Keko na Segerea watasikiliza, yataendelea kuahirishwa kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video Conference) ili kuepuka msongamano na mkusanyiko wa mahabusu na wafungwa mahakamani.

Pia, alisema Kanda ya Mbeya na Bukoba zina vifaa vya mahakama mtandao, utaratibu unakamilishwa kwa uwekaji wa vifaa hivyo katika Magereza yaliyopo katika kanda hizo ili huduma hiyo ianze mara moja.

"Juhudi za kuweka vifaa hivyo kwa kanda zingine zilizosalia zinaendelea na baada ya muda mfupi huduma kama hizo zitatolewa, utumiaji wa mfumo wa usajili wa kesi kwa njia ‘E-Filing’ (kielektroniki). Mahakama inaimarisha na kuwasisitiza wadau wote (wananchi, mawakili wa serikali na mawakili wa kujitegemea) kusajili kesi kwa njia hii ya mitandao ili kupunguza msongamano na mchanganyiko wa watu katika maeneo ya mahakama," alisema Jaji Kiongozi, Dk. Feleshi.

Alisema muhimili huo utaongeza wigo wa matumizi ya Tehama kwa njia ya barua pepe na simu za mkononi kwa kutumia mfumo wa 'SMS notification' na 'USSD' katika usambazaji na upatikanaji wa taarifa za mashauri ambao hautawalazimu wadaiwa kufika mahakamani kupata taarifa hizo.

Mahakama itakuwa ikiendesha programu ya elimu ya namna ya kusajili mashauri, kupata taarifa pamoja na kutoa msaada wa usajili wa kesi kwa njia ya kielektroniki kwa kuanza na mahakama zenye kesi nyingi ambazo zinaweza kusababisha mkusanyiko wa watu wengi.

Naye Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, alisema wanatumia Mahakama Mtandao kwa lengo la kupunguza maambukizi ya corona.

Vile vile, ameshawaagiza mahakimu kupunguza idadi ya watu wakati wa usikilizwaji kesi katika vyumba vya mahakama na badala yake zitumike kumbi za wazi.



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger