Thursday 26 March 2020

Waziri Mkuu: Kamati Za Maafa Ziungane Na Waratibu Wa Kukabiliana Na Corona

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza kamati za Maafa katika ngazi za mikoa na wilaya ziungane na waratibu wa kupambana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) waliopo katika maeneo yao.

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza Watanzania waendelee kujikinga na ugonjwa huo kwa kuhakikisha wanajiepusha na misongamano isiyokuwa ya lazima na hata wakienda kwenye maeneo ya kutolea huduma kama sokoni, vituo vya mabasi wapeane nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 26, 2020) wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Kitaifa cha Kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. Kikao hicho kimehusisha wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipeleke wataalamu katika maeneo yenye mahitaji makubwa kama kwenye viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na bandarini.

“Lengo letu ni kuhakikisha nchi inabaki salama hivyo Watanzania tuendelee kuwa na tahadhari ya kutosambaa kwa ugonjwa huu na pale tunapokwenda kwenye maeneo ya kutolea huduma tujipe nafasi kati ya mtu mmoja na mwingine.”

Waziri Mkuu amesema kamati hiyo inatakiwa ifuatilie na isimamie vizuri ili kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini wanapimwa na wanafuatilia ili kujua historia zao za safari katika kipindi cha siku 14, lengo likiwa ni kuzuia maambukizi hayo yasisambae kwa jamii.

Amesema watu wote waliopewa dhamana ya kuratibu zoezi la kupeleka watu walioko kwenye karantini, wahakikishe wahusika wanafika kwenye hoteli walizozichagua. Pia Serikali inafanya utaratibu wa kutenga maeneo ambayo watu watakuwa wanakaa bila gharama na yatakuwa na huduma zote muhimu.

Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona, ambapo amevitaka viendelee na utaratibu huo kwani utasaidia wananchi kupata elimu na kuweza kujikinga na maabukizi hayo.

Machi 23, 2020, Waziri Mkuu aliunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi ya corona (COVID-19).

Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo inaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Wengine ni Waziri Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Pia, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Msemaji Mkuu wa Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika kikao cha leo, Waziri Mkuu ameongeza wajumbe wawili ili waongeze nguvu katika kukabiliana na virusi vua corona ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger