Saturday, 2 November 2019

Wabadhilifu, Wezi wa Dawa za Serikali Wapewa ONYO Tena

...
Na. Atley Kuni- TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Dorothy Gwajima, ameapa kwamba moto dhidi ya wabadhilifu wa dawa aliouwasha katika zoezi la ufuatiliaji hautazimika wala kupoa, huku akiwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa karibu kwa kuwafichua watu/mtu yeyote atakayebainika kuhujumu jitihada za serikali.

Gwajima ametoa kauli hiyo ikiwa ni mara ya pili kurudia wito huo mbele ya Makatibu Tawala wa Mikoa, wataalamu Wafamasia kutoka mikoa 13 na wadau wa maendeleo Global Supply chain, waliokutana mjini Dodoma kwenye ukumbi wa Mikutano wa OR-TAMISEMI katika kikao kazi cha tathmini ya mbinu mpya ya kuimarisha takwimu za bidhaa za afya.

Akizungumza katika kikao hicho Gwajima amesema, vita hiyo wataweza kuishinda kwa kuunganisha nguvu na wananchi kutoka maeneo yote nchini.

“Niwaombe wanachi kuwa mstari wa mbele kufichua wale wote mtakaowabaini wanahujumu suala la dawa kwani vita hiyo siyo ya mtu mmoja mmoja wala serikali peke yake bali ni ya jamii nzima” alisema Gwajima na kuongeza kuwa, “wapo watu wanaotambua nani ni adui wao katika vita hivi ndiyo maana jana nimeona kwenye Jamiiforum wakinipa pole na kunipongeza, lakini nasema lazima tutembee na wananchi katika hili.” alisisitiza kiongozi huyo.

Gwajima alisema inashangaza unafika kwenye kituo ambacho kina wafamasia wasiopungua sita (6) lakini unakuta kitabu cha kupokelea dawa (ledger) hakijahuishwa kwa zaidi ya miezi 5, hii ni hali ya hatari sana, suala hilo halivumiki na wala hawezi kukubaliana nalo.

“Viongozi wangu Makatibu Tawala, mnaelewa tunatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015-2020, hivyo fuatilieni hili hadi kwenye stoo za kutunzia dawa lakini pia ombeni taarifa na ingieni kwenye mikutano yao muone kile wanachokijadili maana humo hakuna zuio lolote kwa kuwa taarifa zinazojadiliwa humo sio siri za mgonjwa, sasa wasije wakajifichia kwenye mwamvuli wa taarifa za kitabibu kwa kuwahadaa eti siri za Mgonjwa?” Alihoji na alikemea  

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Global Supply Chain Tukay Mavere aliwataka wachumi, watawala wa fedha pamoja na watumiaji wa mfumo wa eLMIS kukaa pamoja na kuja na mbinu mbadala za kudhibiti hali ya dawa na upatikanaji wake na kutoa mrejesho wa kile ambacho serikali imewekeza.

“Lengo la mfumo huu tunataka tuwe tunachukua jambo, tunalichakata na kisha tunalitolea majibu kwa wakati sio kungoja muda uende, aidha hii inakuwa ni zoezi endelevu katika utendaji wa siku kwa siku kama mfumo ulivyo, hivyo tumeitana ili tuwe na uwelewa wa pamoja juu ya hili tunalokusudia kulifanikisha” alisema Mavere.

Kwa upande wao washiriki wa warsha hiyo wameipongeza serikali na wadau kuja na mfumo huo, kwani ni matumaini yao utakuwa suluhu ya yale wanayofanyia kazi kila siku.

“Kama Naibu Katibu Mkuu alivyosema, mfumo huu utasaidia kuondoa ziada ya dawa inayosababisha upotevu wa pesa kutokana na kuchina kwa Bidhaa zilizoingizwa bila takwimu sahihi, vema sasa kila mmoja wetu akitoka hapa awe mstari wa mbele katika kuutumia mfumo kwenye utendaji wake.” alisema, Msalika Makungu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora.

Katika kikao hicho cha siku mbili pamoja na mambo mengine yatakayojitokeza, wataalam watajifunza kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kufanyia maoteo kwa kuwa mfumo unaanzia chini kwenye huduma kwenda juu, hivyo itakuwa ni fursa ya kuwajengea uwezo timu za uratibu wa afya za Mikoa na Wilaya, kupata taarifa sahihi na kufanya ugawaji wa dawa kulingana na mahitaji na kuondokana na tatizo la dawa kwenye maeneo yenye dawa nyingi.

Mambo mengine ni kufanya bajeti kulingana na rasilimali zilizopo lakini pia kuwezesha kufanya usimamizi kwa njia ya mtandao Online Supervision.

Katika kikao hicho, Wataalamu hao walikumbushwa juu ya viapo vyao kwa kuongozwa na kiapo mbele ya Naibu Katibu Mkuu huku wakiwa wamenyoosha mikono juu na kuapa kwamba, watakuwa chachu ya mapambano dhidi ya ubadhilifu wa dawa na endapo wakishindwa basi wawe tayari kuachia nyadhifa zao hata kwa kutuma ujumbe wa maandishi kwenye mtandao wa kundi sogozi (WhatsApp) kuhusu  kuachia madaraka waliyonayo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger