Friday, 29 November 2019

Waziri Mkuu: Madhehebu Ya Dini Yameisaidia Serikali Kupata Viongozi Wazuri

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema madhehebu ya dini yametoa mchango mkubwa katika kuwapata viongozi wa Serikali wanaofuata maadili mema na miiko ya uongozi.

Akizungumza  wakati alipofungua Msikiti wa Haq – Kionga ulioko Magomeni, jijini Dar es Salaam leo mchana (Ijumaa, Novemba 29, 2019), Mheshimiwa Majaliwa amesema imedhihirika kwamba waumini wazuri wa dini mbalimbali wamebainika kuwa ni viongozi wazuri na waadilifu ndani ya Serikali.

Amewasihi viongozi wa dini waendelee kuwafundisha maadili mema waumini wao ili Taifa liendelee kuwa na raia wema ambao baadhi yao ndiyo watakakuwa viongozi katika ngazi mbalimbali hapo baadaye.

“Nyumba za ibada ndiyo mahali sahihi panapojengwa maadili mema kwa watu wa rika zote, hivyo nawaomba Watanzania wawe waumini wazuri wa dini zao kwani kwa kufanya hivyo watakuwa pia ni raia wema,” amesema Mheshimiwa Majaliwa.

Amesema wazazi na walezi wanawajibika kuwarithisha watoto wao imani za dini vizuri kwani anaamini kwa kufanya hivyo watoto watajengewa misingi mizuri ya imani ya dini na maadili mema na watakapokuwa watu wazima watakuwa ni raia wema.

Mheshimiwa Majaliwa aliwasilisha mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli wa sh. milioni 10 na yeye pia alichangia sh. milioni tano ili zisaidie katika awamu ya pili ujenzi wa msikiti huo.

Naye Sheikh Masoud Jongo ambaye alimwakilisha Sheikh Mkuu wa Tanzania katika ufunguzi wa msikiti huo, alisema uhuru mkubwa wa kuabudu uliopo nchini ndiyo sababu kubwa inayoifanya Tanzania iwe ni nchi ya amani na utulivu.

Sheikh Jongo amewaomba Watanzania wautumie vizuri uhuru mkubwa wa kuabudu uliopo nchini kwani ni nchi chache duniani zinazotoa uhuru mkubwa wa kuabudu kwa wananchi wake kama ilivyo hapa Tanzania.

Baadhi ya viongozi walioshiriki katika ufunguzi wa msikiti huo ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia na mbunge wa Kibaha Vijijini, Abuu Juma.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, NOVEMBA 29, 2019.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger