Saturday 30 November 2019

Chuo Cha Mipango Chatakiwa Kufanya Utafiti Wa Umasikini Na Utekelezaji Miradi Ya Umma

...
Benny Mwaipaja, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amekitaka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kutafiti kwa kina namna wananchi wanavyoweza kuondokana na umasikini wa kipato pamoja namna Miradi mbalimbali ya Serikali inavyoweza kutekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha kuliko ilivyo sasa.

Dkt. Kijaji ametoa rai hiyo wakati akiwatunuku astashahada na shahada mbalimbali wahitimu 3,182 Wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi ya Dodoma wakati wa sherehe za mahafali ya 33 ya chuo hicho.

Amesema kuwa matokeo ya tafiti hizo yataisaidia Serikali na Jamii kwa ujumla kupanga mikakati ya namna ya kukabiliana na umasikini wa wananchi hususan wa vijijini pamoja na kuharakisha maendeleo ya nchi kwa kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa na Serikali inakuwa na tija.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti Bw. Pius Mponzi amemwahidi Dkt. Ashatu Kijaji, kwaniaba ya Baraza la Chuo hicho kwamba wataongeza jitihada katika eneo la utafiti na kuhakikisha kuwa matokeo ya utafiti huo yanawafikia wananchi kwa lugha rahisi

Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya amesema chuo chake kimetimiza miaka 40 tangu kianzishwe na kimepata mafanikio makubwa kwa kutoa wahitimu mahili na wenye kukidhi mahitaji ya soko.

Amebainisha kuwa Chuo kimeongeza idadi ya kozi kutoka kozi moja mwaka 1980 hadi kufikia kozi 25 mwaka huu, huku idadi ya wanachuo wanaodahiliwa nayo imeongezeka kutoka wanachuo 13 mwaka huo hadi kufikia wanachuo zaidi ya elfu 11 mwaka huu.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger