Thursday, 28 November 2019

Waziri Mkuu: Nchi Yetu Inahitaji Wataalamu Wa Sekta Ya Uvuvi

...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji kupata watendaji wa sekta ya uvuvi kuanzia ngazi ya vitongoji kwani kuna vijiji vina mito, maziwa na baadhi vimepakana na bahari na hivyo kutoa fursa za uvuvi.

“Nchi yetu inahitaji kupata watendaji kuanzia ngazi ya vitongoji kwani vipo vijiji vyenye fursa za uvuvi hivyo vinahitaji maofisa ugani ili waweze kufanya kazi vijijini na katika vitongoji, lengo likiwa ni kuwasaidia wavuvi wadogowadogo wajue namna bora ya kuvua na kuhifadhi samaki,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa kauli leo jioni (Alhamisi, Novemba 28, 2019), wakati akizungungumza na wahadhiri na wanafunzi mara baada ya ziara yake ya kutembelea Kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema hivi sasa Serikali inaandaa mazingira mazuri ya kuendesha sekta ya uvuvi kwa kupata watalaamu wa ngazi mbalimbali watakaoisimamia sekta hiyo.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambayo imejikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda inasisitiza uwepo wa vyuo vya ngazi mbalimbali ili tuweze kupata watalaamu wa kuendesha viwanda vinavyojengwa nchini,” amesema.

Amesema Serikali inawatambua na inawahitaji sana wasomi wanaopata taaluma zao katika vyuo mbalimbali hapa nchini ikiwemo  kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam  ambayo kwa sasa inatumika kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo ya shahada ya awali, kufundishia na kufanya utafiti kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili pamoja na wafanyakazi watafiti.

Waziri Mkuu amesema angependa kuona watafiti na watalaam wanapewa fursa ya kuongoza na kusimamia maeneo mbalimbali yanayohusiana na utafiti walioufanya ili kupata matokeo sahihi na chanya ya utafiti wao.

Amesisitiza kuwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo thabiti ambayo amemkabidhi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Luhaga Mpina ambaye ameyafanyia kazi  na yameleta mafanikio makubwa katika sekta ya uvuvi nchini.

“Hatua ya kwanza ya kuboresha sekta ya uvuvi ilikuwa ni kuwaondoa watumishi wabovu na wasio waamifu  na nafasi zao kuwapa watumishi  wazuri, wenye taaluma ya uvuvi, waaminifu  na wanaojali zaidi maslahi ya Taifa, kazi ambayo imefanywa na Waziri na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,” amesema.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,  Ajira, Kazi ,Vijana na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama amesema Serikali inaitegemea sana Kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  kwa vile watalaam wanaopata taaluma zao katika kampasi hiyo wanahitajika sana katika maendeleo ya uvuvi nchini.

 Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda ambavyo vitatumia malighafi inayopatikana nchini ikizalishwa na Watanzania wenyewe na bidhaa zake kuuzwa ndani na nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewahakikishia Watanzania kuwa hivi sasa idadi ya samaki na mapato ya Serikali yanayotokana na uvuvi yameongezeka.

Amesema kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kazi ya usimamizi wa  na udhibiti wa uvuvi nchini, mauzo ya bidhaa za uvuvi nje ya nchi yalikuwa ni sh. bilioni  371 kwa mwaka na hivi sasa Serikali inajipatia sh. biloni 691 kwa mwaka.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, NOVEMBA 28, 2019.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger