Wednesday 27 November 2019

Waziri Ummy Atoa Maagizo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii

...
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kusimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa Kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika mikoa na Halmashauri ambazo hazijaanzishwa ili kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia hadi ngazi ya Kata na Vijiji.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsi jana Jijini Dodoma, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimu amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli imetekeleza kwa vitendo azma ya kukomesha vitendo hivyo.

Waziri Ummy ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na asasi za Kiraia katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika maeneo yote hapa nchini.

Aidha, Mhe Ummy ameagiza kuanzishwa kwa Madawati ya Jinsia Katika Taasisi za Elimu ya Juu ili kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono na ukatili mwingine kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi yapatayo 420 yamewezesha wahanga 58,059 kuripoti aina mbalimbali za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa rika mbalimbali wakiwemo watu wazima na watoto katika matukio ya ubakaji, ulawiti, vipigo na ukeketaji.

Akizungumzia faida za madawti hayo Waziri amesema kuwa yameongeza mwamko wa wananchi katika kujiamini na kutoa taarifa za ukatilii unapotokea kwenye maeneo yao.

Kuongeza vituo vya Mkono kwa Mkono vya Kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa Kijinsia (One Stop Centres) kutoka vituo 10 mwaka 2017 hadi 13 mwaka 2019 ili kiwezesha utoaji wa huduma rafiki na kwa haraka kwa wahanga. Hatua hiyo inapelekea Serikali ya Awamu ya Tano kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto 2017/2018- 2021/2022 ambao unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Kauli mbiu ya Kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu ni “Kizazi chenye Usawa: Simama Dhidi ya Ubakaji” kauli mbiu hii inawapa jukumu wananchi wote kutafakari wajibu wao kama kizazi kinachoamini na kuthamini usawa wa kijinsia.

Kauli mbiu hii inatoa msukumo wa kuhakikisha kila mtu katika nafasi yake anapaza sauti na kuchukua hatua ya kuzuia na kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kingono hasa ubakaji na matendo yote ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika nyumba na mahali pa kazi na katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule na vyuo mbalimbali.

Aidha, Serikali inapinga vikali mila, desturi na imani zote zenye madhara kwa jamii kama ukeketaji, kukatisha watoto wa kike shule kwa ajili ya kuolewa.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake Bi Hodan Addou amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupinga vitendo vya ukatili wa Kijinsia kwa makundi yote ili kujenga jamii yenye usawa.

Pia alipongeza juhudi za Serikali katika kuhakikisha inakomesha vitendo hivyo kupitia mpango mkakati wake na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Aliongeza kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni tatizo la kidunia linalohitaji jitihada za pamoja katika kulikomesha.

Uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia umefanyika Jijini Dodoma na umefanywa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na kuhudhudhuriwa na Asasi zisizo za kiserikali, viongozi wa Serikali, Mashirika ya Umma pamoja na Viongozi wa Dini.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger