Tuesday 26 November 2019

Waziri Mhagama Aweka Jiwe La Msingi Ujenzi Wa Kituo Cha Utoaji Wa Huduma Za Ukimwi Ipogolo

...
NA. MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Ipogolo Manispaa ya Iringa ikiwa ni sehemu ya mradi wa uboreshaji wa vituo 20 vitakavyotoa huduma za UKIMWI kwa wasafirishaji wa masafa marefu.

Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 22 Novemba, 2019 katika Kata ya Ruaha Kijiji cha Ipogolo mkaoni Iringa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya ,Omari Badweli (Mb) wa Bahi, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt Leonard Maboko, Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Hamad Ahamad Njovu na wawakilishi kutoka , Ofisi ya Rais -TAMISEMI , Wizara Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano , Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ,TANROADS pamoja na watendaji kutoka Halmashauri.

Kabla ya kuweka Jiwe la Msingi, Waziri Mhagama alipongeza juhudi za Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi za uratibu na utekelezaji wa masuala ya mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuhakikisha ujenzi wa vituo 20 unaanza katika maeneo yenye vichocheo vya maambukizi ikiwemo barabara zinazotumiwa na wasafirishaji wa masafa marefu.

“Uboreshaji wa majengo ya Kituo cha Afya cha Ipogolo kwa niaba ya maboresho kama haya kwenye vituo 20 vilivyoko kando kando ya barabara kuu ya Dar es Salaam hadi mipaka ya Kasumulu (Tanzania/Malawi) na Tunduma (Tanzania/Zambia) ili kutoa huduma za udhibiti wa VVU/UKIMWI kwa ufanisi kwa wasafirishaji wa masafa marefu pamoja na jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo utasaidia kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuzingatia mchango utakaotokana na ujenzi wa vituo hivi”.

Waziri alieleza, ujenzi huo unaotekelezwa kupitia programu ya sattf barabara kuu ya Dar es salaam hadi mipaka ya Tunduma/Nakonde (Zambia) na Kasumulu/Songwe(Malawi) kwa  kutambua umuhimu wa huduma za afya kwa wananchi wa Tanzania na kwa kuzingatia misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) pamoja na marekebisho yake. Uboreshaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ni moja ya utekelezaji wa haki za binadamu katika kupata huduma za afya na haki ya kuishi.

Aidha alieleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi hususani wanaoishi na virusi vya Ukimwi (WAVIU) wanapata haki ya matibabu ya VVU na magonjwa nyemelezi, haki ya kutokubaguliwa na haki za kushirikishwa. WAVIU nao pia wana wajibu wa kulinda wengine wasipate maambukizi ya VVU.

Kwa kuzingatia Sheria ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI (Kuzuia na Kudhibiti) Na. 28 ya mwaka 2008 na Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 zote zinatoa wajibu kwa kila mtu kulinda na kutetea haki za WAVIU.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela akizungumza kwa niaba ya Mkoa wa mkoa huo Mhe.Ally Hapi alieleza kuwa, ujenzi wa vituo hivyo utasaidia kupunguza maambukizi na kuongeza tija katika huduma zitakazotolewa kupitia vituo hivyo.

“Ujenzi wa kituo hiki uwe chachu ya kuendelea kutumia huduma za Ukimwi ikiwemo matumizi sahihi ya dawa za kufubaza virusi ili kuendelea kuwa na afya njema na kushiriki vyema katika shughuli za kimaendeleo nchini’”alisema Kasesela

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa NACOPHA, Leticia Kapela alieleza kuwa, jamii haina budi kuendeea kuunga mkono jitihada hizo na kuhakikisha tatizo la unyanyapaa linatokomezwa kabisa na kuendelea kuishi kwa upendo, usawa na amani.

“Uzinduzi wa leo umeonesha upendo na kujali masuala ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI hiyo niwaombe viongozi wa dini kuungana na jitihada za mapambano haya kwa kuzitumia nafasi zenu kukemea masuala ya unyanyapaa kwa watu wanaosihi na maambukizi.

“Viongozi wa dini tuendelee kuliangalia hili kwa kukemea masuala ya unyanyapaa kwa malengo ya kuifikia 909090 na ikumbukwe hakuna sababu ya kufanya hivyo kwa kuzingatia usemi usemao asohili analile,”alisisitiza Leticia.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger