Monday, 25 November 2019

Mwekezaji Kutoka Malaysia Kuwekeza Mradi Wa Dola Bilioni 2.5 Simiyu

...
Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Mwekezaji Azhar Malik kutoka Nchini Malaysia ameonesha nia ya kuwekeza kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.5 katika mradi mkubwa eneo la pori la akiba la Kijereshi na Ziwa Victoria wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, sehemu ya uwekezaji huo ikiwa ni katika ujenzi wa hoteli ya kitalii, usafirishaji, utamaduni na maeneo mengine yatakayoimarisha utalii na kutoa ajira kwa wananchi.

Mwekezaji ambaye amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhan Dau amesema ikiwa kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa ikiwemo mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari 2020, huku akisisitiza kuwa utatekelezwa bila kuathiri ikolojia na mazingira ya uhifadhi.

“Nashukuru kwa ushirikiano nilioupata kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, pia namshukuru Balozi Dau kwa namna alivyolisimamia jambo hili tangu likiwa wazo mpaka sasa tunapoelekea kwenye utekelezaji niwaahidi tu kuwa pale pande zote zitakapofanya maamuzi mikataba ikisainiwa kwa mujibu wa sheria, mwakani mwezi Januari tutaanza utekelezaji,”alisema Malik

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhan Dau amepongeza uongozi wa Chama na Serikali kwa utayari walioonesha, akisisitiza ushirikiano wa viongozi hao na taasisi zote za Serikali zinazohusika, ili mambo yote muhimu yanayohitajika kufanikisha uwekezaji huo yafanyike mapema  kuanzia mwezi Januari kazi ianze.

“Kwa kasi na namna tulivyoanza lile lengo tulilojiwekea kwamba ikifika Januari 2020 mambo yote yanayohusiana na taratibu na  kusaini mikataba, yanapaswa yawe yamekamilika na wataalam waje site (eneo la mradi) waanze survey (utafiti) watengeneze master plan(mpango kabambe), ili kabla ya mwezi Juni 2020 hili jambo liwe limeanza,” alisema Balozi Dau.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Uwekezaji huu utaupambanua Mkoa wa Simiyu, Kanda ya Ziwa na kuupambanua utalii kwenye uso wa dunia, ambapo amebainisha kuwa mradi huu utajibu mahitaji mengi kwenye ajira na kukua kwa maendeleo ya ukanda huo.

Kwa upande wao Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) wameahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.

Mradi huu wa uwekezaji katika sekta ya utalii wilayani Busega utatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kugharimu takribani dola bilioni 500 na mpaka kukamilika kwake utagharimu dola za Kimarekani bilioni 2.5.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger