Na Abby Nkungu, Singida
Tatizo la kukithiri kwa imani potofu miongoni mwa baadhi ya wananchi kumetajwa kuwa moja ya sababu ya watoto wengi wenye ulemavu kutokupata elimu ya awali kutokana na kufichwa majumbani na wazazi au walezi wao bila kuandikishwa shule hadi wanapokuwa wakubwa.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tumaini Viziwi ya mjini Singida, Francis Edward alibainisha hayo wakati wa mahojiano na Mwandishi huyu juu ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utoaji elimu kwa watoto viziwi.
Alisema kuwa wengi wa watoto hao wenye mahitaji maalum wamekuwa wakifichwa na wazazi au walezi wao kwa imani potofu kuwa hawastahili kusoma na kwamba ni aibu mbele ya jamii inayowazunguka kuwa na mtoto wa aina hiyo; hivyo huwafungia ndani hadi wanapogundulika wakiwa tayari na umri wa miaka 10 hadi 15.
Alieleza kuwa kulingana na Sera ya elimu nchini, haiwezekani kumwandikisha mtoto mwenye umri wa miaka 10 au 15 kwenye masomo ya awali; hivyo uongozi wa shule hulazimika kuwavusha darasa la awali kwa kuwapeleka moja kwa moja darasa la kwanza.
"Hali hiyo inawaathiri kielimu watoto hao kwa kuwa wanakosa msingi muhimu ambao hutolewa katika Shule za Awali ili kumjenga mtoto kiakili na kimwili katika kupokea masomo yake ya madarasa ya juu" alifafanua Mwl Edward.
Alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, tayari wameanzisha mpango maalum wa kuwasaka majumbani watoto viziwi kwa kutumia mbinu na majukwaa mbalimbali katika kuhakikisha wanaandikishwa darasa la awali wakiwa katika umri mdogo kwa mujibu wa Sera ya elimu Nchini.
"Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa shule hii miaka 18 iliyopita, mpango huo umezaa matunda kwa kukusanya watoto 13 tunaotarajia kuwasajili darasa la awali mapema mwakani" alibainisha Mwl Edward.
Alipoulizwa kuhusu changamoto hiyo, Meya wa Manispaa ya Singida, Gwae Chima alisema kuwa atahakikisha anashawishi Mamlaka hiyo kuwa na Sheria ndogo na mahsusi kuwabana wazazi na walezi wenye watoto viziwi ili kuwapeleka shule katika umri mdogo kujiunga na darasa la Awali huku wadau wa elimu wakiunga mkono hoja hiyo.
Wadau hao walisema, inasikitisha kuona katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Sera ya elimu bure na elimu Jumuishi kwa maendeleo ya elimu kwa wote, bado kuna baadhi ya wazazi na walezi wanaoendelea kuficha watoto wao jambo ambalo ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Shule ya Msingi Viziwi Tumaini iliyopo eneo la Karakana mjini Singida ilianzishwa mwaka 2001 na hivi sasa ina wanafunzi 64 kutoka sehemu mbalimbali nchini. Mwaka 2018 ilikuwa miongoni mwa shule 10 bora Manispaa ya Singida zilizofanya vizuri kwenye Mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi.
0 comments:
Post a Comment